The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

NISHATI SAFI YA KUPIKIA NI FUR...

NISHATI SAFI YA KUPIKIA NI FURSA YA KIUCHUMI - MGEJWA.

Watumishi wa Wizara ya Madini wameelezwa kuwa Nishati Safi ya Kupikia ni fursa muhimu ya kiuchumi, kwani pamoja na matumizi ya kupikia, wananchi wanaweza kujipatia kipato kupitia uzalishaji na usambazaji wa Majiko ya Nishati safi ya Kupikia pamoja na vifaa vinavyohusiana na teknolojia hizo.

Hayo yameelezwa Oktoba 13, 2026 na Mjiolojia Mkuu Wizara ya Nishati, Bw. Ngeleja Mgejwa, wakati akitoa mafunzo kuhusu Nishati Safi ya Kupikia kwa watumishi wa Wizara ya Madini katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Katika mafunzo hayo, Mgejwa amewakumbusha watumishi hao malengo mahususi kumi ya Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia, yanayolenga kukabiliana na changamoto zinazokwamisha matumizi ya nishati hiyo nchini.

Amefafanua kuwa malengo hayo ni pamoja na kuongeza uelewa wa wananchi na taasisi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, kuimarisha upatikanaji wa malighafi na miundombinu ya uhakika, kupunguza gharama za nishati safi, vifaa na majiko sanifu ya kupikia pamoja na kuandaa, kuhuisha na kuoanisha sera, sheria, kanuni na miongozo wezeshi.

Malengo mengine ni kuhamasisha uwekezaji, kuongeza wigo wa tafiti na ubunifu wa teknolojia za nishati safi ya kupikia, kujenga uwezo wa utekelezaji wa miradi, kujumuisha masuala ya VVU na UKIMWI na usawa wa kijinsia pamoja na kuimarisha utawala bora katika masuala yanayohusu nishati safi ya kupikia.

Aidha, Mgejwa amewahimiza watumishi hao kuwa mabalozi wazuri wa nishati safi ya kupikia kwa kuhamasisha matumizi yake katika familia, maeneo ya kazi na jamii kwa ujumla, ili kuchangia kufanikisha lengo la Serikali la kufikia asilimia 80 ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi anayeshughulikia masuala ya Afya, Usalama na Utunzaji wa Mazingira wa Wizara ya Madini, Amini Msuya, amewashukuru watoa mada kwa elimu hiyo na kuahidi kuwa Wizara ya Madini itaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia na kuhamasisha matumizi yake katika maeneo ya kazi na jamii kwa ujumla.