NISHATI SAFI YAINGIA SOKONI: WAMACHINGA WAPEWA MAFUNZO MUHIMU.
Wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga wanaofanyia shughuli zao katika Soko la Machinga Complex jijini Dodoma wamepatiwa elimu ya matumizi sahihi ya Nishati Safi ya Kupikia, ikiwa ni hatua muhimu katika kuboresha afya zao na kulinda mazingira.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uelewa wa matumizi ya nishati safi kama gesi, majiko banifu, pamoja na nishati mbadala, ikiwa ni njia ya kupunguza utegemezi wa mkaa na kuni. Washiriki walielezwa kuwa matumizi ya nishati zisizo safi huchangia uchafuzi wa hewa, huongeza hatari ya magonjwa ya mfumo wa upumuaji, na kuongeza gharama zisizo za lazima katika maisha ya kila siku.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mmachinga katika soko hilo, Juma Hassan, alisema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka na yamebadilisha mtazamo wake kuhusu matumizi ya nishati.
“Hapo awali hatukuwa na uelewa wa kutosha kuhusu athari za nishati tulizokuwa tunatumia. Kupitia elimu hii, tumegundua kuwa nishati safi siyo tu inalinda afya, bali pia inapunguza gharama za uendeshaji wa biashara”. Alisema Juma Hassan.
Mbali na mafunzo ya nadharia, washiriki walipata pia mafunzo ya vitendo kuhusu matumizi ya majiko ya kisasa pamoja na mbinu bora za matumizi na uhifadhi wa nishati. Hatua hiyo imewaongezea uelewa na kuwapa ujasiri wa kuanza kutumia teknolojia hizo.
Wamachinga hao wameipokea hatua hiyo kwa matumaini makubwa, wakieleza kuwa matumizi ya nishati safi yatachangia kuboresha mazingira ya kazi, kuongeza tija katika biashara zao, na kulinda mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.