NJIA ZA KUSAFIRISHA UMEME KUWA NGUZO YA KUPELEKA UMEME WA JNHPP KOTE NCHINI – NDEJEMBI.
Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya kusafirisha umeme ili kuhakikisha ongezeko la uzalishaji, hususan kutoka katika Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), linafika kwa uhakika katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza Jumamosi, Agosti 22, 2026, wakati wa hafla ya uzinduzi wa kituo cha kuzalisha umeme cha Julius Nyerere, mgeni rasmi akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Ndejembi amesema kuongeza uwezo wa uzalishaji pekee haitoshi bila kuwa na mtandao imara wa kusafirisha umeme.
“Mheshimiwa Rais, hata hivyo, tunatambua kwamba kuongeza uwezo wa uzalishaji pekee haitoshi. Lazima tuwe na mtandao wenye uwezo wa kupokea na kusafirisha umeme wote kwenda maeneo mbalimbali ya nchi yetu,” amesema Ndejembi.
Amesema mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 400 (kV 400) kutoka Chalinze hadi Dodoma umekamilika na umewezesha umeme unaozalishwa JNHPP kufika Dodoma kwa uhakika zaidi.
Kwa mujibu wa Mhe. Ndejembi, matokeo ya kukamilika kwa njia hiyo yameonekana ndani ya muda mfupi, ambapo kiwango cha juu cha matumizi ya umeme nchini kimeongezeka kutoka megawati 2,130 hadi megawati 2,280 ndani ya siku tatu.
“Ni wiki iliyopita tu, kiwango cha juu cha matumizi ya umeme katika nchi yetu kilikuwa ni megawati 2,130. Lakini mara baada ya kuwasha line ile ya Chalinze–Dodoma, ndio tumefikia sasa kiwango cha juu cha megawati 2,280 hii ni ndani ya siku tatu tu,” amesema.
Ndejembi amesema Serikali pia inaendelea na ujenzi wa njia ya Chalinze–Mkuranga–Kinyerezi kwa lengo la kuimarisha usambazaji wa umeme katika Kanda ya Pwani na maeneo yenye shughuli kubwa za viwanda.
Amesema njia ya TAZA ya Iringa–Mbeya–Tunduma/Sumbawanga yenye urefu wa zaidi ya kilomita 617 imefikia takribani asilimia 98 ya ujenzi, na itaiunganisha Rukwa na gridi ya taifa.
Aidha, amesema ujenzi wa njia ya Songea–Tunduru–Masasi–Mahumbika unaendelea, huku mkandarasi akiwa tayari eneo la mradi, kwa lengo la kuongeza uhakika wa umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Kwa upande mwingine, Serikali inaendelea na upanuzi wa Kituo cha Ibadakuli mkoani Shinyanga, utakaowezesha njia ya kV 220 ya Dodoma–Singida–Tabora–Shinyanga kubadilishwa kuwa kV 400. Hatua hiyo inalenga kuongeza uwezo wa kusafirisha umeme kuelekea Geita, Kanda ya Ziwa na kuunga mkono mradi wa Interconnector ya Tanzania–Uganda.
Tanzania kwa sasa ina uwezo wa kuzalisha megawati 4,646 dhidi ya mahitaji ya juu ya megawati 2,271, huku ikitarajiwa kufikisha megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030 kupitia vyanzo mbalimbali ikiwemo maji, gesi, jua, upepo na jotoardhi.