Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​RAIS ATOA MWAKA MMOJA KWA TAA...

​RAIS ATOA MWAKA MMOJA KWA TAASISI KUPIKIA NISHATI SAFI

RAIS ATOA MWAKA MMOJA KWA TAASISI KUPIKIA NISHATI SAFI

Na Timotheo Mathayo, Dar es salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameagiza Taasisi na Idara za umma na binafsi zenye watu wasiopungua 300 kutumia nishati safi kupikia chakula badala ya kutumia kuni au mkaa.

Ametoa agizo hilo Jumanne Novemba 01, 2022 wakati wafunguzi wa mjadala kuhusu Nishati safi ya kupikia unaofanyika katika ukumbi wa mikutano ya kimataifa wa Julias Nyerere.

Amemuagiza Waziri wa Nishati, January Makamba kuhakikisha idara na taasisi zote za umma na binafsi zenye mkusanyiko wa watu zaidi ya 300 kutumia nishati safi kupika chakula.

"Hili agizo nataka lianze kutekelezwa mwaka 2023/2024. Mwaka huu wote wa 2022/2023 utumike kwa maandalizi ili Shule, Magereza, Majeshi na taasisi nyingine zenye watu wengi zaidi wapike kwa kitumia nishati safi," amesema Rais Samia.

Pia amewaagiza wakuu wa mikoa ya Pwani na Dar es salaam kufanya ukaguzi ili kudhibiti na kukamata watu wanaoharibu vyanzo vinavyopeleka maji mto Ruvu ambao ni chanzo kikuu cha maji katika mikoa hiyo.

"Kuna watu wamechepusha maji na kuingiza katika mashamba yao na wengine wanaingiza maji kwenye mabwawa ya kufugia samaki. Nawaagiza kaondoeni vizuizi vyote vya maji katika eneo la mto Ruvu," amesema Rais Samia.

Mikoa ya Pwani, Morogoro, Ruvuma, Tabora na Lindi imetajwa kuwa vinara wa kuharibu mazingira kwa kukata misitu ovyo, jambo linalochangia kuleta athari za kimazingira katika mikoa hiyo na mikoa jirani.

Awali akimkaribisha Rais Samia kufungua mjadala huo, Waziri wa Nishati, January Makamba amesema kupika sio adhabu, hivyo sio vizuri watu kupika huku wakitokwa machozi kutokana na moshi wa kuni au mkaa.

Alisema kuwa watoto wa kike wapo katika hatari ya mbalimbali kutokana na wao kwenda porini kutafuta kuni za kupikia au kuuza ili wapate kipato cha kaya.

Lengo la mjadala huo ni kutaka jamii iondokane na matumizi ya Nishati isiyo salama, kwa kuwa nishati hiyo ina athari kwa afya ya binadamu, lakini pia inachangia mabadiliko ya tabia nchi na pia imeelekezwa kufikia asilimia 80% ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo Mwaka 2032.