Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​RAIS SAMIA ASHUHUDIA TUKIO LA...

​RAIS SAMIA ASHUHUDIA TUKIO LA UTIAJI SAINI MIKATABA YA UMEME VIJIJINI NA UIMARISHAJI GRIDI

RAIS SAMIA ASHUHUDIA TUKIO LA UTIAJI SAINI MIKATABA YA UMEME VIJIJINI NA UIMARISHAJI GRIDI

Veronica Simba, Zuena Msuya na Issa Sabuni – Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshuhudia tukio kubwa la kihistoria la utiaji saini mikataba ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini pamoja na uimarishaji gridi ya Taifa.

Jumla ya mikataba 14 imesainiwa baina ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Kampuni mbalimbali za Wakandarasi ikihusisha miradi mitatu mikubwa ambayo ni kupeleka umeme kwenye vitongoji 1,522 katika mikoa 9, maeneo 336 ya wachimbaji wadogo wa madini na vituo vya afya, pampu za maji 399 pamoja na kuunganisha wateja wa awali 108,178.

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa upande wake, limeweka saini mikataba 6 kwa ajili ya miradi 26 ya kuimarisha gridi ya Taifa.

Akizungumza katika hafla hiyo fupi iliyofanyika Februari 14, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Samia ameipongeza Wizara ya Nishati, REA na TANESCO kwa kazi waliyoifanya kuwezesha kufikia hatua hiyo ya utiaji saini mikataba ambayo alisema inalenga kuwanufaisha wananchi.

Rais Samia amebainisha kuwa matumaini yake ni kuona miradi husika ikienda kushamirisha uchumi na biashara kwa lengo la kuinua hali ya maisha ya wananchi.

“Huku ndiko kuwajali wanyonge, siyo kusimama kuwaongelea na kuzidi kuwatia unyonge. Tukipeleka umeme wa kutosha kwenye migodi, hali itabadilika kwani wataweza kutumia mitambo bora zaidi katika shughuli zao za uchimbaji na hivyo wataongeza mapato,” ameeleza Rais Samia.

Aidha, amefafanua kuwa umeme katika shughuli za kilimo utawezesha kufanya kilimo cha kibiashara ambacho kina manufaa zaidi kulinganisha na kilimo cha kawaida.

Vilevile, amesema umeme katika vituo vya afya utaboresha zaidi utoaji huduma kwa wananchi hususani kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya akina mama na watoto, ambavyo kwa kiasi kikubwa husababishwa na mazingira duni ya kujifungulia akina mama wajawazito.

Halikadhalika, ameeleza kuwa umeme katika vyanzo vya maji utawezesha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wingi na ubora zaidi.

Akizungumzia Mkakati wa Serikali kupeleka huduma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) maeneo ya vijijini, Rais Samia amesema ili kufanikisha Mpango huo, upelekaji umeme wa uhakika vijijini unatakiwa kwani pasipo nishati hiyo, mkakati husika hautafanikiwa.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amewasisitiza Wakandarasi waliosaini mikataba kufanya kazi kwa bidii na kutimiza makubaliano yaliyofanyika. Amewaonya kuepukana na tamaa zinazoweza kusababisha utekelezaji duni wa kazi.

Pia, amekemea suala la wakandarasi wenye tabia ya kulalamika pale wanaposhindwa kukidhi vigezo na kukosa tenda hali inayowafanya kuzifuata Mamlaka mbalimbali ikiwemo PCCB na PPRA wakitaka ziingilie kati kwa kusimamisha mchakato husika au kuomba urudiwe ili wao wapate tenda hizo.

“Uteuzi wa Wakandarasi unafanywa kwa umakini mkubwa. Ili miradi hii itekelezwe haraka na tupate maendeleo ya haraka, tunahitaji maamuzi ya haraka. Wakandarasi mnaokosa tenda, mkianza kuzunguka PCCB ama PPRA mnazuia miradi na utekelezaji kwenda haraka,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, January Makamba amesema ifikapo Desemba mwaka huu (2023), kila kijiji Tanzania kitakuwa kimefikiwa na umeme.

Hata hivyo, ameeleza kuwa, kufikisha umeme vijiji vyote haimaanishi kuwa ni kusambaza umeme vitongoji vyote. “Unaweza ufikishe umeme vijiji vyote lakini ukawa hujavifikia vitongoji vyote, hivyo nakushukuru Mheshimiwa Rais kutoa maelekezo kuwasilishwa katika Baraza la Mawaziri Mpango wa kupeleka umeme vitongojini,” amebainisha.

Akizungumza zaidi, Waziri Makamba amesema kuwa serikali inatarajia kujenga mradi mkubwa wa umeme wa kuimarisha Gridi ya Taifa ambao utaigharimu serikali shilingi trilioni 4.42 ambao utakamilika ndani ya kipindi cha miaka minne.

Amesema katika mwaka huu wa fedha 2022/2023, serikali imetenga shilingi bilioni 500 ili kuanza utekelezaji wa mradi huo, ambao utakuwa ukitekelezwa kwa awamu tofauti.

“Kukamilika kwa mradi huo itakuwa ni historia kubwa kwa nchi yetu, hasa kwa vizazi vijavyo kuwa kuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika.”

Alisema hadi kufikia mwaka 2025 Serikali inatarajia kufikisha megawati 5000 za umeme nchi nzima.

Akiwasilisha taarifa fupi ya Wakala kuhusu miradi iliyosainiwa, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy alisema kwamba kwa kutambua umuhimu wa uwepo wa nishati bora na endelevu katika maeneo yote yakiwemo ya vijijini, Serikali kwa kushirikiana na Jumuia ya Ulaya na Ufaransa, imetoa Shilingi bilioni 385 ili kuwezesha utekelezaji wa miradi hiyo.

Akitoa takwimu, Mhandisi Saidy alieleza kuwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007, REA imeweza kutekeleza miradi mbalimbali iliyochangia kufikisha huduma ya umeme katika vijiji 9,467 kati ya 12,345 vilivyopo Tanzania Bara sawa na asilimia 76.7 ikiwa ni takwimu za hadi mwezi Januari 2023.

Aidha, aliongeza kuwa vijiji 2,878 vilivyobaki, wakandarasi wanaendelea na shughuli za ujenzi wa miundombinu ya kupeleka umeme kupitia mradi unaoendelea wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili unaotarajiwa kukamilika Disemba mwaka huu wa 2023 na hivyo kufanya vijiji vyote kufikiwa na huduma ya umeme.

“Kwa upande wa vitongoji, kati ya vitongoji 64,760 vilivyopo nchini, vitongoji 28,424 sawa na asilimia 43.9 vilikwishafikiwa na huduma ya umeme. Serikali inaendelea na mipango ya kuongeza mafungu katika Mfuko wa Nishati Vijijini ili kuongeza kasi ya kufikisha umeme katika vitongoji 36,336 vilivyobaki,” alifafanua.

Kuhusu manufaa ya utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini, Mhandisi Saidy alieleza kuwa ni pamoja na kuchangia ipasavyo katika ukuaji wa uchumi katika maeneo ya vijijini, kuboresha huduma za jamii vijijini zikiwemo afya, elimu, maji safi, mawasiliano na usalama pamoja na kuhifadhi mazingira na kuimarisha usalama.

Mkurugenzi Mkuu, kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi na Watumishi wote wa Wakala, alimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kutoa fedha katika kutekeleza miradi ya kusambaza nishati vijijini akifafanua kuwa tangu Serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani, Wakala umesaini mikataba ya miradi mitano yenye thamani ya shilingi trilioni 1.7

“Pia Wakala unashukuru sana uungaji wako mkono kwa juhudi na mipango mizuri ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati katika kuboresha na kuharakisha utolewaji na upatikanaji wa huduma za nishati ya umeme pamoja na nishati safi ya kupikia maeneo mbalimbali nchini,” alieleza Mhandisi Saidy.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Maharage Chande alisema kuwa, ongezeko la mahitaji ya umeme nchini ni asilimia 11 mwaka hadi mwaka, kwa upande wa TANESCO ongezeko hili limekumbana na changamoto nyingi, hivyo kumekuwa na miradi mbalimbali ya kujaribu kuongeza ubora na uhakika wa umeme.

Alisema kuwa, katika miradi ya kuongeza ubora na uhakika wa umeme iliyotekelezwa, hakukuwa na mradi wa kuimarisha Gridi ya Taifa, hivyo mwaka jana walifanya tathmini na kupata kibali cha kuanzisha mradi huo na kuuita Gridi Imara.

Alieleza kuwa, tathmini ya awali ilionesha kuwa mradi wa Gridi Imara unahitaji Shilingi trilioni 4.42 ili kuhakikisha gridi inakuwa ya uhakika na katika mwaka wa fedha 2022/23, Serikali imetenga Shilingi bilioni 500 kwa ajili ya kuanza awamu ya kwanza ambayo ni kati ya Shilingi trilioni 1.9 inayotakiwa kwa awamu yote ya kwanza ili kutekeleza miradi 26 ya kuimarisha gridi nchini.

Aliongeza kuwa, Mradi wote wa Gridi Imara utatekelezwa kwa miaka minne ambapo awamu ya kwanza ambayo mikataba yake imesainiwa, itatekelezwa kwa miaka miwili.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na watu kutoka makundi mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali, viongozi wa dini, wataalamu wa sekta mbalimbali pamoja na wananchi.