Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​​Rasimu ya Muundo wa Mfuko wa...

​​Rasimu ya Muundo wa Mfuko wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia na Miongozo ya Nishati Safi ya Kupikia yajadiliwa na Makatibu Wakuu

Rasimu ya Muundo wa Mfuko wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia na Miongozo ya Nishati Safi ya Kupikia yajadiliwa na Makatibu Wakuu

Makatibu Wakuu kutoka Wizara mbalimbali zinazohusika na masuala ya Nishati Safi ya Kupikia wamefanya kikao ili kupitia rasimu ya muundo wa Mfuko wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia pamoja na taarifa ya uchambuzi wa Sera, Sheria na Mipango inayohusika na Nishati Safi ya Kupikia, ikiwa ni moja ya hatua za kutekeleza lengo la Serikali la kuhakikisha asilimia 80 ya watanzania wanatumia Nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2033.

Kikao hicho kimefanyika jijini Dodoma tarehe 18 Mei, 2023 na kuongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi ambae ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ngazi ya Makatibu Wakuu wanaohusika na masuala ya Nishati Safi ya Kupikia.

Kikao hicho kilijadili rasimu hizo na kutoa maboresho yanayohitajika kabla ya kuziwasilisha katika Kamati ya Mawaziri ya Kikundi Kazi cha Nishati Safi ya Kupikia kupitia kikao kitakachoongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa tarehe 19 Mei, 2023 .

Mhandisi Mramba amepongeza kazi iliyofanywa na Kamati ya Wataalam na Sekretarieti ya Kikundi Kazi na kueleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kutekeleza lengo la kuhamia katika nishati safi ya kupikia ambayo haiathiri afya za binadamu pamoja na mazingira.

Makatibu waliohudhuria Kikao hicho wametoka Wizara mbalimbali ikiwemo Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Wizara ya Afya, na Wizara ya Maliasili na Utalii.