SEKTA YA NISHATI MANENO KIDOGO VITENDO ZAIDI-DKT.BITEKO
SEKTA YA NISHATI MANENO KIDOGO VITENDO ZAIDI-DKT.BITEKO
Ashiriki Bonanza la Nishati jijini Dodoma
Ataka Watumishi kupendana na kushirikiana
Atunukiwa Nishani ya Uasisi Bonanza la Nishati
EWURA yaibuka mshindi wa Jumla;Mkurugenzi Mkuu amshukuru Dkt.Biteko kuthamini Watumishi
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe, Dkt. Doto Biteko amewakumbusha Watumishi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kuiishiKauli Mbiu ya Sekta ya Nishati ambayo ni Maneno KidogoVitendo zaidi ili kuweza kutoa huduma iliyobora kwa wananchi.
Amesema hayo leo tarehe 27 Julai 2024, wakati Watumishi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zilizo chini yake waliposhiriki kwenye Bonanza la Nishati ambalo limefanyika Jijini Dodoma likibebwa na Kaulimbiu Shiriki Michezo Imarisha Afya.
“Sekta ya Nishati ni muhimu kwenye ujenzi wa uchumi wa nchi yetu na tufahamu kwamba Mhe. Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anatutegemea sisi ili kuweza kutoa huduma hii muhimu kwa wananchi, hivyo watumishi tupendane, tushirikiane na kufanya kazi kwa bidi zaidi ili kusukuma mbele gurudumu la Nishati.” Amesema Dkt.Biteko
Kuhusu Bonanza hilo la Nishati, Dkt. Biteko ameeleza kufurahishwa kwake na morali waliyokuwa nayo Watumishi ambao walishiriki kikamilifu katika michezo mbalimbali na kuahidi kuwa huo utakuwa ni utaratibu wa kila mwaka mara baada ya kufanyika kwa Bunge la Bajeti.
Amesema nia ya kufanya Bonanza la Watumishi ni kuhamasishana ili kuweza kutoa huduma bora zaidi kwa watanzania kwa sababu wanaitegema Wizara ya Nishati na Taasisi zake katika kupata huduma hiyo.
Aidha, amewapongeza Watumishi walioshinda michezo mbalimbali katika Bonanza hilo pamoja Viongozi wa Wizara ya Nishati walioratibu Bonanza husika kwa mafanikio.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu , Mhe. Jenista Mhagama ameeleza kufurahinswa na jinsi Bonanza la Nishati lilivyofanikiwa na kusema kuwa huo ni muitikio wa nia ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya ya kuhakikisha Watanzania wanakuwa na afya njema na kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza ambayo dawa yake kubwa ni mazoezi.
Amesema kuwa, michezo inaimarisha afya inajenga umoja, inaleta furaha na kujenga maarifa mapya ya kuwatumikia watanzania hivyo amempongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko kwa kuasisi Bonanza hilo muhimu kwa Watumishi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amemshukuru Dkt.Biteko kwa kuanzishaBonanza hilo ambalo amesema linadumisha upendo miongoni mwa Watumishi, umoja, kuwawezesha wafanyakazi kufahamiana zaidi na kuwaimarisha Watumishi.
Amesema kuwa, anaamini Watumishi wamepata motisha ya kazi kupitia bonanza hilo pamoja na hamasa ya kujipanga na kujiimarisha kwa ajili ya michezo inayofuata.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule naye ameipongeza Wizara ya Nishati kwa kufanya Bonanza hilo mkoani Dodoma hali ambayo imezidi kulifaharisha Jiji la Dodoma na kuchagiza uchumi
Ameahidi kuwa, Serikali mkoani Dodoma itaendelea kuwahamasishawananchi kufanya mazoezi kama ambavyo Viongozi Wakuu wa Nchi wanahimiza ili kuimarisha afya.
Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amemshukuru Dkt.Biteko kwa wazo lake la Bonanza ambalo limeleta hamasa kubwa kwa watumishi na kuahidi kwamba Bonanza hilo sasa litafanyika kila mwaka.
Amesema Taasisi zote chini ya Wizara Nishati zimeshiri ki bonanza hilo ikiwemo Kampuni Tanzu za Taasisi hizo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Dkt. James Andilile ambaye taasisi yake imechukua ushindi wa jumla katika bonanza hilo, pamoja na kumshukuru Dkt. Biteko kwa kuthamini afya za Watumishi, ameeleza kuwa limewawezesha Wakuu wa Taasisi kujadiliana masuala mbalimbali na kupata majawabu ya baadhi ya masuala.
Washindi wa kwanza katika michezo mbalimbali iliyoshindaniwa katika Bonanza hilo ni; Kuvuta Kamba Wanawake (Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC), Kuvuta Kamba Wanaume (TPDC), Volleyball (TANESCO), Mpira wa Pete (TANESCO), Mpira wa Miguu (TANESCO) na mshindi wa jumla ni EWURA.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ametunukiwa nishani ya michezo ikiwa ni kutambua mchango wake katika ufanikishaji wa Bonanza la Nishati huku wazo la kuanzishwa kwa bonanza hilo likianzia kwake.
Baadhi ya Michezo inayofanyika kwenye Bonanza hilo ni Kupokezana vijiti wanaume, Kupokezana Vijiti Wanawake, Rede, Karata, Riadha, Kukimbia na yai, Kukimbia ndani ya gunia, Kukimbia na maji kwenye glasi, Kupenya ndani ya pipa, Mpira wa miguu, Mpira wa Pete, Bao na Karata.