Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​Serikali kuendelea kuimarisha...

​Serikali kuendelea kuimarisha Sekta ya Nishati ili kuvutia wawekezaji zaidi

Serikali kuendelea kuimarisha Sekta ya Nishati ili kuvutia wawekezaji zaidi

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amesema kuwa Serikali itaendelea kusimamia kikamilifu na kuimarisha zaidi Sekta ya Nishati nchini ili kuvutia wawekezaji zaidi katika sekta hiyo na kuondoa changamoto mbalimbali kwenye sekta.

Waziri Mkuu Majaliwa, amesema hayo wakati akifungua Kongamano la Nne la Nishati la Kimataifa katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam, Agosti 3, 2022.

Akizungumza katika Kongamano hilo, Waziri Mkuu Majaliwa amewataka washiriki wa kongamano hilo kujadili fursa zilizopo nchini, wajibu wao,nafasi yao ya kuwekeza nchini, pamoja na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo ili serikali izifahamu na kuzifanyia kazi.

Alisema azma ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ni kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa wawekezaji nchini ikiwemo kuwahakikishia utulivu na amani katika kutekeleza majukumu yao kama sera ya nchi inavyoeleza ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi.

Alisema kuwa Kongamano hilo limesababisha kuwepo kwa mafanikio, na kukua kwa Sekta ya Nishati nchini, hivyo kongamano hilo litaeleza mafanikio yaliyopatikana katika ukuaji wa sekta hiyo nchini.

Ukuaji wa Sekta ya nishati ni pamoja na kuwepo kwa miradi mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanzania, pia ujenzi wa mradi wa kufua Umeme wa Julius Nyerere, ambao unatarajia kuzalisha Megawati 2115 za umeme, ambao utaongeza upatikanaji wa umeme nchini.

“Kongamano hili ni muhimu sana kwa nchi yetu, litafungua fursa za uwekezaji nchini kutokana na kujumuisha makampuni mbalimbali makubwa ya kimataifa katika sekta ya nishati, tuna wageni ambao ni wadau katika sekta ya nishati, hivyo litafungua fursa zilizopo kwenye sekta ya nishati ikiwemo maji, Makaa ya Mawe, Gesi na Umeme wa Jua,”alisisitiza Majaliwa.

Amesema kuwa utekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta ya nishati ikiwemo ya mafuta na gesi itasaidia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi wa nchi kutokana na mapato yatakayokuwa yanakusanywa kutoka kwenye miradi hiyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Januari Makamba amesema Tanzania ina Rais ambaye ana matamanio ya kuifanya sekta ya nishati kuwa chanzo cha ukuaji wa uchumi nchini.

Alilisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na washirika wa kimataifa katika kukuza ushirikishwaji na uwezeshaji wa makundi mbalimbali kiuchumi katika sekta hiyo.

“Lengo la Serikali ni kutumia fursa za sekta yetu ya nishati ili kuboresha sekta nyingine ikiwemo viwanda na uchumi, ninaimani kwamba kongamano hili litawawezesha washiriki kubadilishana uzoefu, mawazo, ujuzi, maarifa, ambayo ni muhimu katika kusimamia rasilimali nishati yakiwemo mafuta na gesi kwa njia sahihi na endelevu kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema Makamba.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha inaweka kanuni na taratibu zinazofaa ili kuwezesha ushirikishwaji wa wafanyabiashara wa ndani kunufaika na mnyororo wa thamani katika sekta ya nishati.

Kongamano hilo limehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Wizara ya Nishati akiwemo Naibu Katibu Mkuu, Kheri Mahimbali, Wakuu wa Taasisi zote zilizochini ya Wizara hiyo, pamoja na Maafisa kutoka Wizara na Taasisi hizo.

Awali, Mkurugenzi wa Ocean Business Partners ambao ndio waandaaji wa kongamano hilo, Balozi Abdulsamad Abdulrahim alisema kongamano hilo litawawezesha wadau kutambua fursa za uwekezaji katika sekta ya nishati nchini

Alisema nchi 89, Watu zaidi ya 1000, makampuni pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya nishati duniani wameshiriki katika Kongamano hilo la siku mbili.