Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​Serikali kujenga Vituo vya Ku...

​Serikali kujenga Vituo vya Kupoza Umeme Katika Wilaya Zenye Uhitaji

Serikali kujenga Vituo vya Kupoza Umeme Katika Wilaya Zenye Uhitaji

Serikali imeendelea na mkakati wa kutekeleza Miradi ya kuimarisha huduma za upatikanaji wa umeme katika wilaya mbalimbali nchini Tanzania.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato wakati akijibu swali la Mbunge wa Igunga, Nicholaus Ngasa aliyetaka kujua ni lini Serikali itajenga kituo cha kupoza umeme cha Igunga.

Swali hilo limeulizwa wakati wa mkutano wa Bunge jijini Dodoma, Septemba 14, 2022.

Byabato amesema kuwa Serikali kupitia TANESCO imebaini uhitaji wa vituo vya kupoza umeme katika Wilaya zenye uhitaji huo, pia imeweka mpango wa ujenzi wa vituo hivyo kulingana na uhitaji kuanzia mwaka huu wa fedha 2022/23.

Amesema ujenzi wa kituo kipya cha kupoza umeme cha Igunga kitawekwa katika mpango wa ujenzi wa Vituo vya kupoza Umeme katika mwaka ujao wa fedha.

Ili kuimarisha huduma ya umeme katika Wilaya ya Igunga na Nzega, Serikali inaendelea na mradi wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Lusu kilichopo wilayani Nzega kutoka MVA 15 132/33kV hadi MVA 60 132/33kV na upanuzi huo unategemea kukamilika ndani ya mwaka huu wa fedha 2022/23.