SERIKALI KUUNGANISHA UMEME KWA SHILINGI 27,000 KATIKA MIJI YENYE SURA YA VIJIJI
Serikali imesema itaendelea kuwaunganishia umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 wananchi wanaoishi katika maeneo ya miji yenye sura ya vijiji yanayokidhi vigezo vilivyowekwa, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme kwa gharama nafuu.
Hayo yameelezwa leo, Oktoba 28, 2026, na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, wakati akijibu swali la Mbunge wa Karagwe, Mhe. Innocent Bashungwa, aliyetaka kufahamu sababu za wananchi wa maeneo ya Mamlaka za Miji ya Kayanga na Omurushaka kutozwa shilingi 320,000 kwa ajili ya kuunganishiwa umeme badala ya shilingi 27,000.
Akifafanua kuhusu suala hilo, Mhe. Salome amesema Wizara ya Nishati imefanyia kazi maombi ya wananchi wanaoishi katika maeneo ya miji yenye sura ya vijiji, ambapo jumla ya maeneo 2,292 yametambuliwa nchini kote kwa kuzingatia vigezo mbalimbali, ikiwemo hali halisi ya kiuchumi ya wananchi wanaoishi katika maeneo hayo.
Ameeleza kuwa katika Miji ya Kayanga na Omurushaka, maeneo yaliyobainishwa na kukidhi vigezo hivyo ni Kagururu-Kabingo, Rwambale, Karaizo, Kayanga Majengo Mapya, Katahoka, Kilimahewa, Galilaya, Tuwaka, Omgakorongo, Nyakanongo, Kashakamba, Golani, Kamahungu, Nyakahama, Karundu, Nyakahanga Nyarutuntu, Nyakahanga Akitoma na Kishao.
Aidha, amesema kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 1020 la mwaka 2020, linalosimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), gharama za kuunganisha umeme wa njia moja (Single Phase) hutofautiana kulingana na kundi la eneo husika. Wananchi wa vijijini walio ndani ya mita 120 kutoka kwenye njia ya umeme hulipa shilingi 27,000, huku wananchi wa mijini walio ndani ya mita 30 wakitozwa shilingi 320,960.
Mhe. Salome amefafanua kuwa maeneo ya Mamlaka za Miji ya Kayanga na Omurushaka yanakidhi vigezo vya kundi la maeneo ya mjini vilivyoainishwa katika Jedwali Na. 5 la Sheria ya Mipango Miji Na. 8 ya mwaka 2007.
Vilevile, amesema utambuzi wa maeneo ya miji yenye sura ya vijiji umetokana na hoja zilizowasilishwa na Waheshimiwa Wabunge wakati wa uwasilishaji wa Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2026/27, mwezi Aprili 2026, ambapo waliomba wananchi wa maeneo hayo wawezeshwe kupata huduma ya umeme kwa gharama ya shilingi 27,000.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwawezesha wananchi wanaoishi katika maeneo ya miji yenye sura ya vijiji yanayokidhi vigezo vilivyowekwa kuunganishiwa umeme kwa gharama ya shilingi 27,000, kwa kuzingatia hali halisi ya kiuchumi ya wananchi katika maeneo husika.