Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​SERIKALI YAAHIDI KUANZA MRADI...

​SERIKALI YAAHIDI KUANZA MRADI WA KUZALISHA UMEME WA RUMAKALI.

SERIKALI YAAHIDI KUANZA MRADI WA KUZALISHA UMEME WA RUMAKALI.

Na Timotheo Mathayo, Dodoma.

Serikali imeahidi kuanza ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Rumakali katika wilaya ya Makete mkoani Njombe utakaozalisha Megawati 222 baada ya kukamilika.

Mradi huo utatekelezwa kupitia Shirika la umeme nchini (TANESCO) ambapo maandalizi ya utekelelezaji wa mradi huo yameanza kwa hatua za awali.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato wakati akijibu swali la Mbunge wa Makete, Festo Sanga aliyetaka kujua ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Bwawa la umeme katika Mto Rumakali.

Swali hilo limeulizwa wakati wa mkutano wa Bunge uliomalizika Jijini Dodoma, Ijumaa Septemba 23, 2022 ambapo Byabato alisema kuwa Serikali imetenga sh. bilioni 8 kwa ajili ya maandalizi ya awali ya mradi huo katika mwaka wa fedha 2022/2023.

"TANESCO imehuisha upembuzi yakinifu pamoja na nyaraka za zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi mjenzi wa mradi huo", alisema Byabato.

Uthamini wa mali za wananchi zitakazopitiwa na mradi huo utakamilika mwezi Oktoba, 2022 ili kuwezesha wananchi kulipwa fidia, hivyo utekelezaji wa mradi huo wa kuzalisha umeme unatarajia kuanza mwaka wa fedha 2023/2024.

Byabato alisema kuwa mradi wa kuzalisha umeme wa Rumakali utakapokamilika utawanufaisha wakazi wa Makete pamoja na maeneo mengine ya nchi kwa kuwa utaunganishwa kwenye gridi ya Taifa.

Byabato alisema Serikali inaendelea kujenga vituo vya kupoza umeme katika maeneo mbalimbali nchini ili kuweza kukabiliana na tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara.