The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

SERIKALI YAONGEZA KASI UTEKELE...

SERIKALI YAONGEZA KASI UTEKELEZAJI WA MKAKATI WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA.

Serikali imeendelea kuongeza kasi ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia kupitia mipango mbalimbali inayolenga kuhakikisha wananchi wanapata na kutumia nishati safi ya kupikia.

Hayo yameelezwa na Mhandisi kutoka Wizara ya Nishati, Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia, Mhandisi. Anitha Ringia, wakati akiwasilisha mada katika Kongamano la Siku ya Nishati (Energy Day) linalofanyika sambamba na Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Amesema Serikali imeendelea kutekeleza mkakati huo kupitia jitihada mbalimbali ikiwemo utoaji wa ruzuku, kuondoa kodi kwenye mita janja (smart meter) za gesi ya LPG pamoja na baadhi ya bidhaa za LPG, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji na matumizi ya nishati hiyo kwa wananchi wengi zaidi.

Mha. Ringia amesema kupitia jitihada hizo, Serikali imefanikisha usambazaji wa majiko ya gesi 452,445 kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini, huku majiko banifu 200,000 nayo yakisambazwa ili kuongeza upatikanaji wa teknolojia salama na bora za kupikia.

Katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwenye taasisi zinazotoa huduma ya chakula kwa watu wengi, Mha. Ringia amesema hadi sasa jumla ya taasisi 1,472 zimehamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia, huku lengo likiwa ni kuhakikisha taasisi 31,395 zinafikia matumizi hayo katika kipindi cha utekelezaji wa mpango huo.

Ameongeza kuwa mafanikio ya Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia yanategemea ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, sekta binafsi, washirika wa maendeleo, taasisi za kifedha, asasi za kiraia na wananchi, ili kufanikisha azma ya Taifa ya kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuboresha ustawi wa jamii.