The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

TABWA YAAHIDI KUSHIRIKIANA NA...

TABWA YAAHIDI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUENDELEA KUTOA ELIMU YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA.

Jumuiya ya Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TABWA) imesema itaendelea kushirikiana na Serikali kutoa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia mafunzo yanayofanyika katika mikoa mbalimbali nchini.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa TABWA, Bi. Noreen Mawalla, Juni 25, 2026 wakati wa hafla ya kufunga Maonesho na Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia (Nishati Safi Expo 2026) lililofanyika katika Ukumbi wa EACLC, Ubungo jijini Dar es Salaam.

Bi. Mawalla alisema kongamano hilo ni endelevu na hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini hivyo kuwafikia wananchi wengi zaidi kupitia programu mbalimbali za elimu.

Aidha, amewashukuru wadau, washiriki na wadhamini wa kongamano hilo lililofanyika kwa siku tatu akisema mchango wao umewezesha kufikiwa kwa malengo ya kutoa elimu na kujenga uelewa kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Bi. Mawalla alisema uamuzi wa kuendelea kutoa elimu umechochewa na takwimu zinazoonesha athari za kiafya na vifo vinavyotokana na matumizi ya nishati zisizo safi.

Amebainisha kuwa kongamano hilo limekuwa jukwaa muhimu la kujifunza na kubadilishana uzoefu kupitia mawasilisho kuhusu matumizi salama ya nishati safi ya kupikia, tahadhari za matumizi ya gesi na uhifadhi wa mazingira, huku akihimiza makundi yote ya jamii kuendelea kutumia nishati safi kwa manufaa ya afya, mazingira na maendeleo endelevu.