TANESCO, Watanzania wanataka Umeme- Dkt. Biteko
TANESCO, Watanzania wanataka Umeme- Dkt. Biteko.*
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema watanzania wanataka umeme na hivyo kuwataka Viongozi na Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO kufanya kila jitihada za kuhakikisha kunakuwa na nishati ya uhakika.
Ameyasema hayo leo Septemba 13, 2023 Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Wafanyakazi wa Shirika hilo na kuongeza kuwa zinahitajika jitihada za dhati za kuhakikisha kunakuwa na rasilimali watu ya kutosha pamoja na mahusiano mazuri kazini hatua ambayo itaboresha utendaji kazi wa shirika hilo.
*“Watanzania wanataka umeme, hata tungekuwa na mipango ya namna gani watanzania wanachotaka ni umeme, unaweza kusema fulani anafanya hivi, au mchakato wa kupata rasilimali fedha kwa ajili ya kunua kifaa fulani unaenda hivi lakini watanzania hayo hawayajui, wao wanamjua TANESCO ndio mleta umeme, katika kazi zetu na Taasisi nyingine za Serikali moja ya mambo tunayotakiwa kufanya ni kuzingaunisha taasisi nyingine ili tuweze kuwafikia watanzania kwa haraka, na kazi hii ni ya kwetu”* amesema Dkt. Biteko.
Amewataka Viongozi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati kushughulikia mambo badala ya kushughulika na watu hali ambayo ameitaja kuwa inavunja ari ya kufanya kazi.
*”Kama viongozi mtawagawanya wafanyakazi kwenye makundi, mahali pa kazi patakuwa pagumu kwa sababu mtakuwa mmekusanya genge la soga na wapiga majungu kazini, na mwisho watanzania hawatapata umeme, wafanyeni watu hawa kuwa ni daraja linalofanana na kama tutashughulika na masuala binafsi ya watu badala ya masuala ya kazi hatutafikia malengo, kuna watu wanahofu ya mabadiliko, na hali hiyo tunaitengeneza sisi viongozi, kwa sababu ukiingia mahali badala ya kushughulika na jambo unaanza kushughulika na watu, na wafanyakazi wote hawa maisha yao yote ya utumishi wao masaa mengi wanatumia wakiwa kazini, hawa ni binaadamu, kuna wakati watakuwa wamekwazwa, wamevunjika moyo. Mahali wanapofanyia kazi kuwe ni kimbilio kwao.”* amesema Dkt. Biteko.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba amemuhakikishia Dkt. Biteko kuwa Wizara yake kupitia shirika la TANESCO inafanya kila jitihada za kuhakikisha watanzania wanapata huduma bora na za uhakika za Nishati ya Umeme.
*Mhe. Waziri, nikuhakikishie kwamba Wizara yetu tunafanya juhudi zote za kuhakikisha watanzania wanapata umeme wa uhakika, na tunatafanya haya kwa sababu Serikali yetu inatuwezesha kwa kila namna”* amesema Mhandisi Mramba.
8:42 AM (3 minutes ago) | |||
|