Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

TANZANIA KUNUFAIKA NA FURSA ZA...

TANZANIA KUNUFAIKA NA FURSA ZA UWEKEZAJI WA MIRADI YA JOTOARDHI

“TANZANIA KUNUFAIKA NA FURSA ZA UWEKEZAJI WA MIRADI YA JOTOARDHI”

Tanzania itanufaika na Mpango wa kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya Jotoardhi na teknolojia za kisasa ili kuleta maendeleo endelevu. Mpango huo unatekelezwa na Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa (UNIDO) unahusisha nchi sita (6) ambazo ni Tanzania, Djibouti, Ethiopia, Kenya, Rwanda na Uganda.

Hayo yamebainika wakati wa Jukwaa la Mpango wa Kuendeleza Jotoardhi kwa nchi za Ukanda wa Mashariki ya Afrika lililofanyika nchini Japan tarehe 18 hadi 24 Julai, 2023.

Akichangia mjadala wa ushirikishwaji wa Sekta Binafsi katika uendelezaji wa Jotoardhi kwa nchi za Afrika, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu wa Wizara ya Nishati Mha. Innocent Luoga alisema Tanzania ipo tayari kushiriki katika Mpango wa UNIDO wenye lengo la kuhamasisha matumizi ya nishati ya jotoardhi pamoja na kuwajengea uwezo Wataalam wake kwa nchi za Ukanda wa Mashariki ya Afrika.

“Tupo tayari kushirikiana na Mashirika ya Kimataifa, Washirika wa Manedeleo, Sekta Binafsi na Wadau wa nishati ya Jotoardhi katika kuendeleza rasilimali ya jotoardhi nchini Tanzania.”

Mha. Luoga alieleza kuwa Tanzania ina maeneo zaidi ya 50 yenye rasilimali ya jotoardhi ambayo yana uwezo wa kuzalisha umeme takribani megawati 5,000. Aliyataja baadhi ya maeneo ni Ngozi na Kyejo Mbaka yaliyopo mkoani Mbeya, Luhoi (Pwani), Songwe, Kisaki (Morogoro) na Natron (Arusha). Aidha, alieleza hatua mbalimbali iliyofikiwa katika uendelezaji wa maeneo hayo na faida za kutumia nishati hiyo ambayo ni rafiki wa mazingira.

Kamishna Luoga alitumia jukwaa hilo kuwakaribisha Wadau wote wa Jotoardhi kushiriki katika Kongamano la 10 la Jotoardhi la Nchi za Ukanda wa Mashariki ya Afrika (African Rift Geothermal Conference – ARGeo C10) litakalofanyika Novemba, 2024, Dar es Salaam, Tanzania. Tanzania iliteuliwa kuwa mwenyeji wa Kongamano hilo katika Mkutano wa Kongamano la 9 lililofanyika Nchini Djibouti, Mwezi Novemba, 2022.

Katika ziara hiyo nchini Japan, Wizara ya Nishati pamoja na Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) zilipata fursa za kufanya vikao na mashirika mbalimbali yanayofadhili miradi ya jotoardhi duniani ili kupata fedha na misaada ya kiufundi kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo. Aidha, Ujumbe huo wa Tanzania ulipata nafasi ya kutembelea Mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia Jotoardhi wa Hatchobaru (HGPP) ambao unazalisha megawati 110.

Kamishna Luoga aliambatana na Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Nishati Bw. Petro Lyatuu, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Kuendeleza jotoardhi nchini (TGDC) Prof. Shubi Kaijage na Kaimu Meneja Mkuu wa TGDC, Mha. Mathew Mwangomba.