The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

TANZANIA KUZALISHA MEGAWATI 13...

TANZANIA KUZALISHA MEGAWATI 130 ZA JOTOARDHI KUFIKIA 2030

Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema katika kuendeleza nishati ya jotoardhi, Tanzania inaendelea na shughuli za utafiti ikiwemo katika eneo la Ziwa Ngozi lilipo wilayani Rungwe mkoani Mbeya ili kuhakikisha inazalisha megawati 130 za jotoardhi ifikapo mwaka 2030.

Mhe Ndejembi ameyasema hayo Januari 11, 2026, Abu Dhabi katika Falme za Kiarabu kwenye mjadala wa Baraza la Kimataifa la Nishati Jadidifu (IRENA) uliohusu matumizi ya Nishati ya Jotoardhi kwa ajili ya kuzalisha umeme na matumizi mengineyo ikiwemo Kilimo, Uvuvi, Viwandani na katika Utalii.

Pamoja na Jotoardhi, Mhe Ndejembi ameeleza kuwa Tanzania pia inaendeleza vyanzo vingine vya nishati jadidifu ikiwemo jua na upepo ambapo kupitia mradi wa umeme jua wa Kishapu megawati 150 zitazalishwa na kuingizwa kwenye gridi ya Taifa.

" Pamoja na changamoto tunazokabiliana nazo katika hatua ya awali ya utafiti ya uendelezaji wa nishati hii ya jotoardhi, Tanzania tunaendelea na utafiti eneo la Ziwa Ngozi ambapo kwa ujumla tumepanga kuzalisha megawati zipatazo 130 za jotoardhi ifikapo mwaka 2030.

Hivyo nitoe wito kwa sekta binafsi na wadau wa maendeleo kushirikiana na Serikali katika hatua za awali za utafiti kwa ajili ya uendelezaji wa Nishati ya Jotoardhi kwani Tanzania pekee inavyo vyanzo takribani 52 vinavyoweza kuzalisha megawati 5000," Amesema Waziri Ndejembi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kimataifa kutoka Benki ya Dunia, Dkt. Demetrios Papathanasiou amesema Benki ya Dunia inayo nia ya kufadhili hatua za utafiti na uendelezaji wa nishati ya Jotoardhi nchini Tanzania ili kuwezesha nishati hiyo kuwa na mchango mkubwa katika uzalishaji wa umeme kama ilivyo kwa nishati nyingine kama vile Maji na Gesi Asilia.

Katika mikutano hiyo ya IRENA, Waziri Ndejembi ameambatana na Kaimu Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Bakari Ameir, Kamishna Msaidizi anayeshughulikia Nishati Jadidifu, Mhandisi Imani Mruma pamoja na wataalamu wengine kutoka Wizara ya Nishati.