Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​TANZANIA MWENYEJI KONGAMANO L...

​TANZANIA MWENYEJI KONGAMANO LA 10 LA JOTOARDHI MWAKA 2024

TANZANIA MWENYEJI KONGAMANO LA 10 LA JOTOARDHI MWAKA 2024

Tanzania itakuwa mwenyeji wa Kongamano la 10 la Jotoardhi la Nchi za Ukanda wa Mashariki ya Afrika (African Rift Geothermal Conference - ARGeo) litakakofanyika Mwaka 2024.

Hayo yameelezwa katika Kongamano la 9 la Jotoardhi la Nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati lililofanyikatarehe 3 hadi 5 Novemba, 2022 katika Mji wa Heron nchini Djibouti ambalo lilijadili uendelezaji wa nishati ya Jotoardhi katika kuzalisha umeme na matumizi mengine.

Akimwakilisha Waziri wa Nishati kwenye Kongamano hilo, Kamishna Msaidizi wa Umeme Mha. Innocent Luoga alisema “tupo tayari kuwa wenyeji wa Kongamano la 10 la Jotoardhi litakalofanyika Mwaka 2024 ili tuweze kupata manufaa ya kongamano hilo ikiwa pamoja na kuharakisha kupata umeme unaotokana na Jotoardhi.”

Mhandisi Luoga alieleza kuwa, pamoja na kuimarisha ushirikiano na nchi wanachama, Tanzania itanufaika na kongamano hilo kwa kuhamasisha uendelezaji wa Jotoardhi nchini, kupata fedha za kutekeleza Miradi ya Jotoardhi, pamoja na kubadilishana uzoefu na nchi zilizofanikiwa katika kuzalisha umeme kwa kutumia Jotoardhi zikiwemo Kenya na Ethiopia.

Katika Kongamano hilo, Wizara ya Nishati pamoja na Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) zilipata fursa za kufanya vikao na Mashirika mbalimbali yanayofadhili Miradi ya Jotoardhi ili kupata fedha za kutekeleza Miradi hiyo. Mashirika hayo ni pamoja na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA), Mfuko wa Kuzuia Athari za Jotoardhi (GRMF) na Benki ya Maendeleo ya Biashara ya Afrika (TDB).

Kamishna Luoga aliambatana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya kuendeleza Jotoardhi nchini (TGDC) Prof. Shubi Kaijage, Kaimu Meneja Mkuu wa TGDC, Mha. Mathew Mwangomba, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa TGDC Mha. Shakiru Kajugus pamoja na Mjumbe wa Kamati ya ARGeo Mha. Kato Kabaka.