Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

TANZANIA, ZAMBIA WAKUTANA KUJA...

TANZANIA, ZAMBIA WAKUTANA KUJADILI USALAMA BOMBA LA MAFUTA

TANZANIA, ZAMBIA WAKUTANA KUJADILI USALAMA BOMBA LA MAFUTA

Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba, ameongoza ujumbe wa Mawaziri wa Tanzania wakiwemo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Viongozi Waandamizi wa Serikali pamoja na Mawaziri wa Zambia wakiwemo, Waziri wa Ulinzi, Mhe. Ambrose Lufuma, Waziri wa Nishati, Mhe. Peter Chibwe Kapala, Waziri wa Mambo ya ndani na Usalama wa Nchi, Mhe. Jacob, Jack Mwiimbu katika mkutano wa kujadili namna ya kuongeza Ulinzi na Usalama wa Bomba la Mafuta la Tanzania-Zambia Crude Oil Pipeline (TAZAMA Pipeline) mara baada ya kubadilisha matumizi kutoka kusafirisha mafuta ghafi hapo awali, ili kusafirisha mafuta ya dizeli.

Hii ni matokeo ya kikao cha Rais wa Tanzania Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zambia Mhe. Hakainde Hichilema ambapo marais hawa walikubaliana kuwa, Mawaziri husika wa pande zote mbili wakutane ili kuhakikisha usalama wa bomba la Mafuta la TAZAMA unazingatiwa.

Leo mawaziri hao wametekeleza maagizo ya wakuu wa nchi hizo mbili ikiwa ni katika kuenzi maono ya Hayati baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Rais wa kwanza wa Zambia Hayati Kenneth David Kaunda katika kudumisha mahusiano ya kindugu yenye lengo la kukuza uchumi wa nchi hizo mbili ikiwemo suala la bomba la TAZAMA.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Hyatt Regency Hotel jijini Dar es Salaam leo, Mhe. January Makamba ameeleza kuwa mara baada ya Serikali ya Zambia kubadilisha matumizi ya bomba hilo kutoka kusafirisha mafuta ghafi ili kusafirisha mafuta ya dizeli, bomba hilo kwa sasa litahitaji ulinzi zaidi ili kulinda usafirishwaji wa mafuta hayo suala lililopelekea umuhimu wa viongozi wa pande zote mbili kukutana na kujadili usalama wa bomba hilo.

"Kama mnavyofahamu, Tanzania na Zambia zina ushirikiano wa muda mrefu ulionzishwa na marais waasisi wa nchi hizi mbili, ambao pia unahusisha bomba la mafuta la TAZAMA. Kati ya nchi hizi mbili, huko nyuma bomba la TAZAMA lilikuwa linasafirisha mafuta ghafi. Hata hivyo, miaka kadhaa iliyopita Serikali ya Zambia iliamua kubadilisha matumizi ya bomba hilo ili lisafirishe mafuta ya dizeli.

Uamuzi huo umepelekea haja ya kuimarisha usalama katika maeneo yote yanayopitiwa na bomba hilo ikihusisha pia wananchi wanaoishi jirani na bomba hilo pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi zote mbili. Hii ni kutokana na thamani ya bidhaa itakayokuwa ikisafirishwa kupitia bomba hilo, kwa kuwa ukishaanza kusafirisha mafuta ya dizeli maana yake usalama wa bomba lenyewe unakuwa ni jambo kubwa la kuzingatiwa.

Hii ni kutokana na kuwa, suala la usalama katika mafuta ghafi lilikuwa si hatarishi sana kama tunavyokwenda kwenye kusafirisha mafuta ya dizeli. kwa hiyo sasa tukaamua Serikali zetu mbili kufanya uratibu wa usalama wa bomba " Amesema Mhe. Makamba"


Kwa upande wake Waziri wa Nishati wa Zambia,Mh. Peter Chibwe Kapala ameeleza kuwa, awali walikuwa wanasafirisha mafuta ghafi kutoka Tanzania kwenda Zambia ambako yanachakatwa. Gharama za uendeshaji zilikuwa kubwa na Serikali yao ilikuwa ikitumia ruzuku kubwa katika uendeshaji.

Hivyo, sasa wamefanya mabadiliko ili bomba hilo litumike kusafirisha mafuta ambayo tayari yameshachakatwa ( Dizeli) lakini pia ni wakati wa kufikiria ikiwezekana, waweze kujenga bomba la kusafirisha gesi kutoka Tanzania kwenda Zambia hali itakayosaidia kupunguza ukataji miti hovyo kwa ajili ya mkaa na kuni na kuwezesha kutunza mazingira.

Naye Waziri wa Ulinzi wa Zambia, Mhe. Ambrose Lufuma ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo pamoja na timu ya ufundi kwa kufanya kazi nzuri ndani ya siku mbili walizokaa pamoja ambapo, wameweza kuja na mipango mbalimbali itakayotumika kulinda bomba hilo ikiwemo ufungaji wa kamera za CCTV, matumizi ya drones na kuweka askari kwa ajili ya ulinzi wakati wote.

"Sote tunafahamu kuwa bomba la TAZAMA lilikuwa linabeba mafuta ghafi ambayo yalikuwa hayavutii kama haya ya sasa ambayo yatakuwa yameshachakatwa. Hivyo, tunahitaji kulilinda bomba hili na ndiyo maana tuko hapa kujaribu kuona jinsi tutakavyolilinda. Tumepokea mawazo mbalimbali na tunaendelea kuzungumza juu ya kuongeza ulinzi, ili kuwezesha kuwepo kwa usalama wa bomba masaa ishirini na nne. Tutaweka drones na kamera za ulinzi (CCTV camera) hii yote ni kulitunza na kulilinda bomba hili."Amesema Mhe. Lufuma