TPDC YAISHUKURU SERIKALI, SHELL NA EQUINOR KWA KUKAMILISHA UJENZI WA SHULE YA MSINGI LIKONG’O.
Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imetoa shukrani za dhati kwa Wizara ya Nishati, Serikali ya Mkoa wa Lindi, pamoja na kampuni za Shell na Equinor kwa ushirikiano wao uliofanikisha kukamilika kwa ujenzi wa Shule ya Msingi na Awali ya Likong’o mkoani Lindi kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa shule hiyo, Oktoba 26, 2026, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC, Balozi Peter Kallaghe, amesema shule hiyo ni sehemu ya mchango wa Shirika katika kuboresha huduma za kijamii, pamoja na ishara ya shukrani na heshima kwa wananchi wa Likong’o ambao walikubali kwa hiari kuachia maeneo yao ili kupisha utekelezaji wa Mradi wa Kimkakati wa Gesi Asilia ya Kimiminika (LNG).
Amesisitiza kuwa mafanikio ya TPDC hayapimwi kwa utekelezaji wa majukumu yake ya msingi pekee, bali pia kwa mchango wake katika kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo endelevu katika maeneo yanayozunguka miradi ya mafuta na gesi asilia.
Aidha, amesema Bodi ya Wakurugenzi itaendelea kusimamia utendaji wa Shirika kwa ufanisi ili kuongeza tija katika sekta ya petroli na gesi asilia, huku ikihakikisha kuwa miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii inazalisha manufaa ya moja kwa moja na yanayoonekana kwa wananchi wa Lindi na Watanzania kwa ujumla.
“TPDC inaamini kuwa ushirikiano thabiti kati ya Serikali, wawekezaji wa sekta binafsi, Shirika na wananchi ndio msingi muhimu wa kufanikisha maendeleo jumuishi na endelevu,” amesema Kallaghe.
Kukamilika kwa Shule ya Msingi na Awali ya Likong’o kunatarajiwa kuimarisha upatikanaji wa huduma za elimu katika eneo hilo, kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, pamoja na kuandaa kizazi chenye maarifa na ujuzi kitakachoshiriki kikamilifu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Lindi na Taifa kwa ujumla.