The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

TUMIA KWA KADRI ULIVYOLIPIA: T...

TUMIA KWA KADRI ULIVYOLIPIA: TEKNOLOJIA YA MGAS LPG YAFANYA NISHATI SAFI YA KUPIKIA KUFIKIKA KWA WENGI ZAIDI.

Kampuni ya Mgas LPG imeendelea kutoa mchango mkubwa katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini kupitia teknolojia ya Smart Meter, mfumo unaomwezesha mtumiaji kufuatilia kiwango cha gesi kilichosalia kulingana na matumizi yake ya kila siku.

Teknolojia hiyo pia huipa kampuni uwezo wa kupata taarifa mapema kabla gesi haijaisha, hatua inayoongeza ufanisi wa huduma na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa gesi kwa wateja.

Akizungumza katika Maonesho ya Mkutano wa Nishati Safi ya Kupikia unaoendelea jijini Arusha, Mkuu wa Maendeleo ya Biashara na Ukuzaji wa Mgas LPG, Bw. Abdallah Kijangwa, alisema mfumo huo umebuniwa mahsusi kuondoa changamoto za gharama za awali zinazowazuia wananchi wengi kuanza kutumia gesi ya kupikia.

Alieleza kuwa kupitia mfumo wa “Tumia kwa Kadri Ulivyolipia”, mteja anaweza kupata jiko kwa gharama nafuu na kulipia kidogo kidogo kwa shilingi 7,500 kwa mwezi kwa kipindi cha miaka miwili. Aidha, mteja hupatiwa mtungi wa gesi pamoja na kifaa cha Smart Meter bila gharama za ziada.

“Teknolojia hii inampa mteja uhuru wa kununua gesi kulingana na uwezo wake wa kifedha wakati wowote. Hii imeongeza unafuu na kurahisisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa kaya nyingi”. Alisema Bw. Kijangwa.

Aliongeza kuwa mfumo huo humwezesha mtumiaji kujua kiwango cha gesi kilichobaki wakati wowote na kutoa taarifa mapema kabla gesi haijaisha, jambo linalosaidia kuondoa usumbufu wa kukatizwa kwa huduma na kuhimiza matumizi endelevu ya gesi ya kupikia.

Kwa mujibu wa Bw. Kijangwa, hadi sasa Mgas LPG imefanikiwa kufikia zaidi ya kaya 12,500 zinazotumia huduma zake. Alisema kampuni inaendelea na mikakati ya kupanua huduma katika mikoa mbalimbali nchini ili kuongeza idadi ya watumiaji wa nishati safi ya kupikia na kuchangia utekelezaji wa ajenda ya Taifa ya nishati safi.