Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​TUMIENI FURSA YA UMEME KWA SH...

​TUMIENI FURSA YA UMEME KWA SHUGHULI ZA MAENDELEO - NAIBU WAZIRI BYABATO

TUMIENI FURSA YA UMEME KWA SHUGHULI ZA MAENDELEO - NAIBU WAZIRI BYABATO

Naibu Waziri Nishati, Mhe. Wakili Stephen Byabato amefanya uzinduzi wa Mradi wa kusambaza umeme vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili kimkoa mkoani Simiyu katika kijiji cha Igwata kata ya Nyabubinza wilayani Maswa .

Naibu Waziri Byabato alisema tarehe 08/07/2021 kuwa, jumla ya vijiji 151 kwa mkoa mzima vitapatiwa huduma ya umeme ambapo Wilaya ya Maswa ni vijiji 13, Bariadi 35, Meatu 48 na Busega vijiji 4 pamoja na vijiji vyote amabavyo havijafikiwa na huduma ya umeme pia vitafikiwa vyote bila kubakiza hata kimoja.

Naibu Waziri Byabato aliwataka wananchi kushirikiana na Serikali ili kutoa ardhi na maeneo yao ili miundombinu ya umeme ipite ili waweze kupata huduma ya umeme na kuboresha maisha yao na huduma za kijamii.

Alisisitiza kuwa, bei ya umeme ni shilingi 27,000 kwa wateja wanaohitaji njia moja ya kusafirishia umeme (single phase) na 139,000 kwa wateja wanaohitaji njia tatu za kusafirishia umeme (Three phase).

Aliwasisitiza wananchi kuchangamkia fursa hiyo ya kuunganishiwa umeme ambayo ni kichocheo muhimu cha maendeleo.

Aidha, Mhe. Byabato alimuagiza Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili kuwasha umeme katika kijiji cha Igwata ndani ya mwezi mmoja kuanzia leo tarehe 08/07/2021.

Kwa upande wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)) Naibu Waziri wa Nishati, aliliagiza kufunguliwa kwa madawati ya kutolea huduma ili kuwasaidia wananchi kutopata usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kulipia huduma ya umeme.

Aliwasisitiza wananchi kushirikiana na TANESCO ili kuwaongoza kupata wakandarasi wanaofunga umeme majumbani ili kukwepa kutapeliwa na vishoka.

Naibu Waziri Byabato aliwashauri wananchi ambao bado hawapo tayari kuweka mtandao wa nyaya katika nyumba zao kutumia kifaa cha UMETA (Umeme tayari) ambacho mwananchi atafungiwa kwa 27,000 tu.