Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

UJENZI WA MRADI WA BOMBA LA MA...

UJENZI WA MRADI WA BOMBA LA MAFUTA LA HOIMA UNASHIRIKISHA WAZAWA MKOANI KAGERA

#Wakandarasi na watoa huduma 42 wapatiwa kazi

Dodoma

Imeelezwa kuwa ujenzi wa Mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga unashirikisha wakandarasi wazawa kutoka mkoani Kagera.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga, kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu kutoka mkoani Kagera Mhe. Neema Kichiki Lugangira aliyetaka kujua je ni wakandarasi wangapi kutoka mkoani Kagera wamepata kazi katika mnyororo wa ujenzi wa bomba la mafuta la Hoima mkoani Tanga.

Mhe. Kapinga amesema kuwa wakandarasi wakuu wa Mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga wanaendelea kushirikiana na wakandarasi wadogo, wajenzi na watoa huduma mbalimbali katika mikoa yote inayopitiwa na Mradi.

Mhe. kapinga aliongeza kuwa jumla ya wakandarasi na watoa huduma 42 wamepata kazi mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa ujenzi wa Mradi huu ikiwemo uuzaji wa vifaa vya ujenzi, huduma za usambazaji wa mafuta, huduma za umeme na hoteli.