Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​UJENZI WA NJIA YA KUSAFIRISHA...

​UJENZI WA NJIA YA KUSAFIRISHA UMEME KATIKA MRADI WA JNHPP YAFIKIA ASILIMIA 92

UJENZI WA NJIA YA KUSAFIRISHA UMEME KATIKA MRADI WA JNHPP YAFIKIA ASILIMIA 92

Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba amesema kuwa, Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) inaendelea na utekelezaji wa mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Bwawa la Julius Nyerere hadi Chalinze pamoja na ujenzi wa Kituo cha kupoza umeme cha Chalinze ambapo ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya kV 400 imefikia asilimia 92.

Makamba amesema hayo Machi 12, 2023 wakati Wizara ya Nishati ilipotoa taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Bwawa hilo la kuzalisha umeme hadi Chalinze kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini jijini Dodoma.

“Utekelezaji wa miradi hii ipo katika hatua mbalimbali, mradi wa njia ya kusafirisha umeme yenye msongo wa kilovoti 400 imefikia asilimia 92 na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Chalinze ambacho kinahusisha ufungaji wa Mashine umba sita umefikia asilimia 55.” Amesema Makamba

Amefafanua kuwa, mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ambapo njia hiyo ya kusafirisha umeme ina urefu wa kilomita 160 na ujenzi wa Kituo cha kupoza Umeme cha Chalinze inahusisha ufungaji wa Transfoma Sita.

''Mradi huu unagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, gharama ya mradi ni Dola za Marekani milioni 51.5 na shilingi bilioni 39.12 ambapo ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme utatumia kiasi cha Dola za Marekani Milioni 44.06 na Shilingi Bilioni 30.85 zinatumika kwa ajili ya kujenga kituo cha kupoza umeme cha Chalinze," Amesema Makamba.

Ametaja Mkandarasi wa mradi wa kusafirisha umeme kuwa ni Larsen & Toubro Limited kutoka India na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Chalinze unatekelezwa na Mkandarasi TBEA kutoka China.

Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Bunge, Mhe.. Dunstan Kitandula ameipongeza Serikali kwa jitihada ya utekelezaji wa miradi mbalimbali katika Sekta ya Umeme, Gesi na Mafuta ikiwemo mradi wa ujenzi wa Bomba la Mafuta ghafi la Afrika Mashariki.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Kamishina wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga na watendaji wengine kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).