UKATAJI WA HEKTA 469,420 ZA MISITU KWA AJILI YA KUNI NA MKAA WAATHIRI MAZINGIRA.
Mhandisi Benezeth Kabunduguru, Mtaalamu kutoka Wizara ya Nishati, Kitengo cha nishati safi ya kupikia, Agosti 13, 2026, ametoa elimu kwa Waheshimiwa Madiwani wa Manispaa ya Mpanda kuhusu athari za matumizi ya nishati zisizo safi za kupikia na umuhimu wa kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amesema takribani hekta 469,420 za misitu hupotea kwa mwaka kutokana na shughuli za kibinadamu, ikiwemo upatikanaji wa kuni na mkaa, hali inayochangia uharibifu wa mazingira.
Ameeleza kuwa upotevu wa misitu unachangia kuongezeka kwa ukame na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo kuongezeka kwa joto pamoja na mvua kutokuwa na mpangilio.
Aidha, amesema uharibifu wa misitu unaathiri mifumo ya kiikolojia, ikiwemo kupungua kwa viumbe walio katika hatari ya kutoweka.
Mhandisi Kabunduguru amesisitiza umuhimu wa Madiwani kutumia nafasi zao kuhamasisha wananchi kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwemo gesi, umeme, biogesi na teknolojia nyingine rafiki kwa mazingira.
Ameeleza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yatasaidia kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, hivyo kuchangia katika uhifadhi wa misitu na mazingira kwa ujumla.
Mafunzo hayo kwa Waheshimiwa Madiwani yamefanyika katika mikoa mitatu Simiyu, Singida na Katavi, yakilenga kuwajengea uwezo kuhusu athari za matumizi ya nishati zisizo safi za kupikia na kuwapa uelewa wa nafasi yao katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia katika maeneo yao.