Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​Usambazaji Gesi majumbani iwe...

​Usambazaji Gesi majumbani iwe ni kipaumbele-PAC

Usambazaji Gesi majumbani iwe ni kipaumbele-PAC

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, imetoa wito kwa Serikali kuwa, suala la usambazaji gesi majumbani liwe ni la kipaumbele.

Wito huo umetolewa kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe.Naghenjwa Kaboyoka jijini Dar es Salaam mara baada ya ziara ya Kamati hiyo kutembelea miundombinu mbalimbali ya Gesi iliyopo mkoani Mtwara, Pwani na Dar es Salaam.

Alisema kuwa usambazaji wa Gesi hiyo majumbani uzingatie kupeleka nishati hiyo kwenye maeneo yenye watu wengi ili kuweza kupunguza matumizi makubwa ya mkaa ambayo yanapelekea ukataji wa miti na hivyo kuleta uharibifu wa mazingira.

Kuhusu ziara ya Kamati hiyo kwenye miundombinu ya Gesi alisema kuwa, Kamati imeona uwekezaji mkubwa uliofanyika na kufurahishwa na jinsi wafanyakazi watanzania wanavyoendesha na kusimamia miundombinu hiyo kwa ufanisi mkubwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio aliieleza Kamati hiyo kuwa, kazi ya usambazaji Gesi majumbani inaendelea katika mikoa mbalimbali na kwamba ili gesi hiyo isambazwe kwa wananchi wengi zaidi, wameanza kukaribisha kampuni binafsi ili ziweze kusambaza nishati hiyo majumbani.

Ziara ya PAC ilikuwa na malengo mbalimbali ikiwemo kuona kama ujenzi wa miundombinu ya Gesi iliyopo inalingana na thamani ya fedha iliyotolewa.

Wajumbe wa PAC walitembelea mitambo ya kuchakata gesi ya Mnazi Bay ambapo Gesi hiyo husafirishwa kwenda Mtwara Mjini ili kuzalisha umeme unaotumika katika mikoa ya Mtwara na Lindi na Gesi nyingine hupelekwa kwenye mitambo ya kuchakata Gesi ya Madimba inayomilikiwa na TPDC.

Aidha, Kamati hiyo pia ilitembelea visima vya gesi vitano vilivyopo nchi kavu katika eneo hilo la Mnazi Bay mkoani Mtwara, nyumba zilizounganishwa na Gesi Asilia kwa ajili ya kupikia na matoleo ya Bomba kubwa la Gesi ambayo hupeleka Gesi maeneombalimbali ikiwemo kiwanda cha Saruji cha Dangote kilichopo mkoani Mtwara.

Aidha, wajumbe hao wa Kamati walitembelea mitambo ya kuchakata Gesi Asilia iliyopo Madimba yenye uwezo wa futi za ujazo milioni 210 ambapo gesi hiyo baada ya kuchakatwa husafirishwa kwa Bomba kubwa linalotoka eneo hilo mpaka mkoani Dar es Salaam na hivyo kuwezesha gesi hiyo kutumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kuzalisha umeme, kutumika viwandani kwenye magari na majumbani.

Vilevile Wajumbe hao walitembelea vituo vya kupokea Gesi iliyochakatwa vya Somanga mkoani Lindi na Kinyerezi jijini Dar es Salaam.

Viongozi mbalimbali waliohudhuria ziara ya Kamati hiyo ni Kamishna Msaidizi wa Gesi, Mohamed Fakihi, akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, DKt.James Mataragio na Kaimu Meneja Mkuu wa GASCO, Baltazary Mrosso.