The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

UWEKEZAJI WA SHILINGI BILIONI...

UWEKEZAJI WA SHILINGI BILIONI 50 KITUO CHA MPOMVU WAIMARISHA UPATIKANAJI WA UMEME KANDA YA ZIWA.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imefanya ziara ya ukaguzi katika Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Mpomvu kilichopo mkoani Geita, Machi 15, 2026, ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya Nishati inayolenga kuimarisha upatikanaji wa umeme nchini.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Subira Mgalu amesema ziara hiyo imelenga kukagua maendeleo ya miradi ya nishati pamoja na kuhakikisha uwekezaji unaofanywa na Serikali unaleta matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi.

“Kama Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini tuna jukumu la kuisimamia Wizara ya Nishati ili kuhakikisha inatekeleza majukumu yake kikamilifu. Tumeridhishwa na uwekezaji uliofanywa katika kituo hiki ambacho kina mchango mkubwa katika kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi na shughuli za kiuchumi,” amesema Mhe. Mgalu.

Ameongeza kuwa Kituo hicho kina uwezo wa kupokea na kusambaza takribani megawati 90, huku jitihada zikiendelea kuboresha miundombinu ya usambazaji wa umeme ikiwemo mpango wa kuongeza laini maalum kwa ajili ya Mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM).

“Mahitaji ya umeme ya mgodi wa GGM yanatarajiwa kufikia takribani megawati 70 ifikapo mwaka 2035 kutoka megawati 36 zinazotumika kwa sasa, hivyo ni muhimu kuendelea kuimarisha miundombinu ya usambazaji wa umeme ili kukidhi mahitaji hayo,” ameongeza.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Salome Makamba amesema Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya umeme katika Mkoa wa Geita kutokana na ukuaji mkubwa wa shughuli za kiuchumi na kijamii hususani katika sekta ya madini.

“Kituo hiki kina mchango mkubwa katika kuimarisha upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Geita pamoja na maeneo ya jirani ikiwemo Biharamulo na Ngara mkoani Kagera, Sengerema mkoani Mwanza na Kakonko mkoani Kigoma,” amesema Mhe. Salome.

Naibu Waziri wa Nishati ameongeza kuwa Kituo cha Mpomvu kimegharimu takribani shilingi bilioni 50, uwekezaji ambao umeongeza uwezo wa usambazaji wa umeme katika eneo hilo linalokua kwa kasi kiuchumi ambapo mahitaji ya sasa ya umeme yamefikia Megawati 73.64.

Awali, Mkoa wa Geita ulikuwa ukipokea umeme kutoka Mkoa wa Shinyanga wenye uwezo wa takribani megawati 4 pekee, kiwango ambacho hakikukidhi mahitaji ya umeme yaliyokuwa yakiongezeka kutokana na shughuli za kiuchumi hususani uchimbaji wa madini.

Kituo cha Kupokea na Kupoza umeme cha Mpomvu kilianza kujengwa mwaka 2019 na kukamilika mwaka 2020, kabla ya kuzinduliwa rasmi mwaka 2022 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.