Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​​VIJIJI 353 VINA UMEME GEITA

​​VIJIJI 353 VINA UMEME GEITA

VIJIJI 353 VINA UMEME GEITA

Serikali imeahidi kuendelea kuimarisha huduma za upatikanaji wa umeme Vijijini ili kuwawezesha Wananchi waishio katika maeneo hayo kuwa na nishati ya uhakika itokanayo na umeme.

Waziri wa Nishati, January Makamba ametoa ahadi hiyo wakati akitoa salamu kwa Wananchi wa Geita kwenye ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan iliyofanyika Oktoba 15, 2022.

Makamba alisema kuwa jumla ya Vijiji 486 vilivyopo katika Mkoa wa Geita ni vijiji 353 vilivyopata umeme na bado 133 tu ila serikali imekwisha wapatia wakandarasi kwa ajili ya shughuli za kuunganisha na kusambaza umeme katika maeneo yaliyobakia ili ifikapo mwaka 2025 kila Kijiji kiwe kimepata umeme.

Alisema kuwa serikali inaendelea na mipango ya kupeleka umeme kwenye migodi ya wachimbaji wadogo wa madini, lengo likiwa ni kupunguza matumizi ya jenereta wakati wa shughuli za utafutaji wa madini.

Makamba alisema kuwa serikali imetenga sh. bilioni 57 kwa ajili ya kupeleka umeme kwenye migodi ya wachimbaji wadogo na kati ya hizo sh. Bilioni 7 ni fedha kutoka kwa wakala wa nishati Vijijini (REA) na Bilioni 50 zimetolewa na TANESCO.

Wakati wa ziara hiyo Rais Samia Suluhu Hassan amekagua na kuzindua kituo cha kupoza umeme chenye uwezo wa kuzalisha megawati 90 kilichopo katika Mkoa wa Geita.

Wizara ya Nishati imeandaa mpango ujulikanao kama Gridi ya magharibi ambao utajumuisha mikoa ya Kanda ya ziwa ikiwemo Geita ili kuwezesha mikoa hiyo kuwa na gridi itakayojitegemea.

Serikali itajenga Vituo vya kupokea Umeme kwa wingi, njia za kusafirisha umeme pamoja na kuzalisha umeme wa kutosha katika Mikoa hiyo.

"Kuna miradi mbalimbali ambayo tayari imepata fedha kama vile Malagarasi, Kakono, Kishapu na Rusumo ambayo inategemea kuzalisha jumla ya megawatt 400 itakapokamilika," alisema Makamba.

Makamba alisema asilimia 90 ya wananchi wa Geita wanatumia nishati yenye sumu kupikia ikiwemo mkaa, kuni na mabaki ya mazao, nishati ambayo inatoa moshi wenye sumu zaidi ya mia mbili na husababishia vifo ambapo watu 33,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na athari za sumu hiyo.

Wizara ya nishati imeandaa mpango wa kuhamasisha matumizi ya Nishati safi ya kupikia ili kuwawezesha wananchi kuondokana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia.