​VIONGOZI WAKUU WASTAAFU WATEMBELEA MRADI WA JULIUS NYERERE


VIONGOZI WAKUU WASTAAFU WATEMBELEA MRADI WA JULIUS NYERERE

Hafsa Omar- Rufiji

Viongozi Wakuu wa Kitaifa Wastaafu Waheshimiwa Marais na Mawaziri Wakuu Wametembelea mradi wa Bwawa la Kufua Umeme wa Maji la Julius Nyerere(JNHPP) unaotekelezwa katika Mto Rufiji kwa lengo la kujionea maendeleo ya mradi.

Viongozi hao wametembelea mradi huu, Julai 5,2021 katika ziara hiyo waliambatana na Mawaziri mbalimbali wakiongozwa na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani na Viongozi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake.

Wakizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kumaliza kukagua mradi, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mhe. Ali Hassan Mwinyi amesema amefurahishwa na namna wataalamu wa kitanzania walivyoweza kusimamia mradi huo kwa ustadi mkubwa hivyo amewapongeza kwa kutumia vema taaluma yao kusimamia ujenzi wa Mradi huo.

Kwa upande wake, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete amempongeza Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa ujasiri wa kuamua mradi ujengwe na kwa kutumia fedha za ndani ili kutimiza ndoto ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.zxxd2a”W0

Ameeleza kuwa, ndoto ya Baba wa Taifa ilikuwa ni kujenga bwawa kubwa la kuzalisha umeme, lenye shughuli ya utalii, litakalopunguza mafuriko sehemu ya chini ya mto Rufiji na kuwezesha kilimo cha umwagiliaji kitakacholisha takribani watu milioni ishirini, na kuwataka wadau wa kilimo kuanza kujipanga kutumia fursa ya kilimo cha umwagiliaji.

Nae, Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. John Malecela, amesema kuwa tangu taifa lipate uhuru halijawahi kutekeleza mradi mkubwa kama huo wa Kufua Umeme kwa Maji na kuwataka Watanzania kulinda mradi huo.

Mhe. Malecela, amesema, watanzania wanapaswa kujivunia na kujisikia fahari kwani mradi huo unasimamiwa na wazawa ambao wameonesha uzalendo kwa taifa kwa kusimamia vema ujenzi wake.

Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya amempongeza Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani na wataalamu wa Wizara ya Nishati kwa kujitoa na kuwajibika kikamilifu katika usimamizi wa ujenzi wa mradi huo.

Nae,Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda, amewataka watanzania kutumia mradi huo vizuri kwasababu utakuwa na fursa nyingi sana ambazo zitawakomboa watanzania kiuchumi.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameleza kuwa hadi sasa mradi umefikia asilimia 54.3 ambapokazi kubwa za msingi zimeshafanyika na asilimia zilizobaki zitakamilika ndani ya miezi michache.

Ameeleza kuwa,tayari mkandarasi ameshalipwa zaidi ya trilioni mbili na sasa Serikali inaendelea na maandalizi ya kuwalipa tena wakandarasi kwa hatua ya ujenzi waliofikia.

Aidha, amesema mradi ukikamilika nchi itakuwa na umeme wa kutosha, wa uhakika na wenye gharama nafuu hivyo ametoa wito kwa wenye nia ya kuwekeza kujitokeza na kuwekeza kwenye shughuli za kilimo, umwagiliaji na utalii.

Vilevile, ameeleza kuwa kupitia uzoefu wa usimamizi wa mradi huo watanzania tumejifunza kwamba hata miradi mingine itakayoanza kutekelezwa itasimamiwa na watanzania wenyewe kwani wataalamu wazawa wanao uwezo huo.