VYOMBO VYA HABARI NI MABALOZI MUHIMU WA KUHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA.
Meneja wa Mradi wa CookFund kutoka Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Mitaji (UNCDF), Emmanuel Muro, amesema Waandishi wa habari na maafisa mawasiliano Serikalini wana nafasi muhimu katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia Watanzania wote na kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi kuhusu teknolojia za kupikia.
Amesema mradi wa CookFund wenye thamani ya Euro milioni 19.4 uliotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano umechangia kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuchochea mahitaji ya wananchi na kuwezesha suluhisho mbalimbali kuwafikia watumiaji wa mwisho ambapo mradi huo umetekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma na Mwanza.
Amefafanua kuwa, mafanikio ya mradi huo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya UNCDF na Wizara ya Nishati, ambapo kwa pamoja wamehakikisha taarifa kuhusu faida za nishati safi ya kupikia zinawafikia Watanzania wengi kupitia kampeni mbalimbali za uhamasishaji na ushirikishwaji wa wadau.
Amesema wananchi wengi bado wana wasiwasi kuhusu gharama za kuanza kutumia nishati safi ya kupikia, hivyo ni jukumu la wanahabari na wataalamu wa mawasiliano kuandaa na kusambaza ujumbe unaoeleza kwa usahihi gharama, manufaa na fursa zilizopo ili kuwawezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi.
Aidha, amesisitiza kuwa uchaguzi wa teknolojia au suluhisho la nishati safi ya kupikia unabaki kuwa hiari ya kila mwananchi kulingana na mahitaji na uwezo wake huku akiwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kuwa mabalozi wa kueneza elimu sahihi kuhusu nishati safi ya kupikia ili kuharakisha kufikiwa kwa malengo ya taifa ya kuongeza matumizi ya nishati hiyo nchini.