WAANDISHI NA MAAFISA MAWASILIANO WAPEWA ZANA ZA KUSUKUMA AJENDA YA NISHATI SAFI.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Nishati, Bi. Nteghenjwa Hosseah, amesema mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea Uwezo Waandishi wa Habari na Maafisa Mawasiliano Serikalini kutoka katika Wizara na Taasisi kuhusu Uandishi na Uhamasishaji wa Masuala ya Nishati Safi ya Kupikia, yameandaliwa ili kuwajengea uelewa na msingi imara utakaowawezesha kutekeleza kwa ufanisi jukumu la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, Bi. Hosseah amesema mafunzo hayo yataimarisha uwezo wa washiriki katika kufikisha ujumbe sahihi kwa wananchi na kuchochea juhudi za kufikia lengo la Serikali la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Aidha, amewataka washiriki kuyafanyia kazi maelekezo na maarifa watakayopata wakati wa warsha hiyo kwa kushirikiana kwa karibu, ili kuendelea kuisukuma mbele ajenda ya nishati safi ya kupikia na kuunga mkono jitihada za Serikali za kulinda afya za wananchi na mazingira.