Wabunge wa Uganda wajifunza usafirishaji wa mafuta ghafi TAZAMA
Wabunge wa Uganda wajifunza usafirishaji wa mafuta ghafi TAZAMA
Na Zuena Msuya, DSM
Serikali kupitia Wizara ya Nishati imepokea Ujumbe kutoka nchini Uganda waliokuja nchini, kuona na kujifunza mambo mbalimbali kuhusu sekta ya Mafuta hasa usafirishaji wa mafuta ghafi kupitia Bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Tanzania hadi Zambia (TAZAMA).
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema hayo wakati wa ziara ya ujumbe huo uliohusisha Wabunge wa Kamati ya Mazingira na Maliasili, ukiongozwa na Waziri wa nchini, anayeshughulikia Maendeleo ya Madini, Wizara ya Nishati na Madini nchini Uganda, pamoja na wataalam mbalimbali nchini humo iliyofanyika Julai 20, 2022 mkoani Dar es Salaam.
Mhandisi Mramba amesema kuwa, ujumbe huo umekuja nchini kwa ziara maalum yenye lengo la kujifunza mambo mbalimbali katika sekta ya nishati, hasa eneo la mafuta kwa kuwa nchi hiyo itaanza kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga hapa nchini, kupitia Mradi wa Bomba la kusafirisha mafuta ghafi (EACOP). Mradi huo unahusisha nchi mbili ambazo ni Uganda na Tanzania.
Alisema kuwa Tanzania inauzoefu wa zaidi ya miaka 50 katika mradi wa kusafirisha mafuta ghafi kupitia bomba la TAZAMA, ambalo limekuwa likisafirisha mafuta hayo kutoka Tanzania hadi Zambia kwa kipindi kirefu, hivyo ni eneo sahihi kwa ujumbe huo kuona na kujifunza.
Pia Tanzania imetekeleza mradi wa bomba la kusafirisha Gesi Asilia kutoka Mkoani Mtwara hadi Kinyerezi, mkoani Dar es Salaam inayotumika kuzalisha umeme unaongizwa katika Gridi ya Taifa.
Aidha Tanzania ipo katika mazungumzo ya awali ya kujenga bomba kubwa la kuzafirisha gesi asilia kutoka Mtwara hadi nchini Uganda, hivyo ni wakati sahihi kwa wajumbe hao kujifunza na kuona ili wakati wa kutekeleza miradi hiyo ukifika iwe rahisi kwa wao kuulekeleza uzoefu walioupata na kutoa maoni yao.
“Ujio wa ujumbe huu wakiwepo wabunge wa Kamati ni muhimu sana,kwa kuwa wao ndiyo wanaosimamia mambo mbalimbali na kuishauri serikali ya Uganda, ni vyema wakafahamu zaidi yale mambo yanayoamuliwa na serikali ili yaweze kupita kwenye ngazi ya wabunge, ni wakati sahihi kwao kuja kuona na kujifunza kile kinachoendelea kufanyika kutika bomba la TAZAMA ” alisema Mhandisi Mramba.
Ziara hiyo pia imeshirikisha Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Tanzania,Dunstan Kitandula Kamishna Msaidizi Mafuta na Gesi wa Wizara ya Nishati, Michael Mjinja na viongozi wengine waandamizi kutoka wizarani na taasisi zilizochini yake.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi anayeshughulikia maendeleo ya Nishati na Madini wa Uganda, Mhandisi Peter Lokeris aliishukuru Serikali ya T anzania kwa kukubali mradi wa bomba kupitishwa katika ardhi yake, alisema hiyo imeonyesha dhahiri kuwa nchi hizo zina mahusiliano mazuri licha ya kuwa ni majirani.
Mhandisi Lokeris alisema kuwa serikali yatanzania kuruhusu bomba hili kusafirisha mafuta yao itawasaidia kuinua uchumi wa nchi yao kwakuwa watatumia gharama ndogo kusafirisha mafuta hayo ukilinganisha na usafirishaji kwa kutumia njia zingine kama magari, pia nchi hizo mbili zitanufaika n mradi ktokana na faida itakayopatikana kupitina.
Sambamba na hiyo usafirishaji wa mafuta hayo utatumia muda mfupi na salama zaidi kwa bidhaa hiyo, utunzaji wa miundombinu ya barabara pamoja na kulinda uharibifu wa mazingira.
“Tumekuja kujifunza Tanzania kwa sababu wenzetu hawa ni wazoefu wa miaka mingi katika miradi hiyo mikubwa, ukiachana na hili la mafuta la TAZAMA ambalo lina zaidi ya miaka hamsini, wanalile la gesi na katika miaka yote hii hakuna siku tumesikia changamoto yoyote hivyo umekuja kwa lengo maalum la kupata uzoefu” alisema Mhandisi Lokeris
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya bunge Nishati na Madini, Dunstan Kitandula kwa upande wa Tanzania na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mazingira na Maliasili wa Ufanda, Otiam Otaala kwa pamoja wamesema kuwa ziara za namna hiyo kwa wabunge ni muhimu sana kwakuwa wabunge watafahamu zaidi nini kinaenda kufanyika kwakuwa wao ndiyo wenye wanadhamana kubwa ya kuhakikisha kuwa miradi yenye tija kwa taifa na wananchi inatekelezeka kwa wakati.
Pia kama washauri wa serikali na wawakilishi wa wananchi, ni wajibu wao kufahamu kwa undani masuala mbalimbali yanayofanyika na yatakayofanyika ili kwa nafasi zao waweze kuishauri serikali namna bora ya kutekeleza na kufikisha ujumbe sahihi kwa wananchi wanaowawakisha.
Ziara hiyo ya kujifunza imefanyika wakati sahihi kwakuwa Uganda sasa imeanza kutekeleza mradi wa bomba la kusafirisha mafuta, na bado inaendelea na tafiti mbalimbali ili kuibua miradi mingine mikubwa.