Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

Wakandarasi wa mradi wa REA II...

Wakandarasi wa mradi wa REA III mzunguko wa Pili watakiwa kwenda maeneo ya kazi

Na Teresia Mhagama, Dodoma

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amefanya kikao kazi na wakandarasi kutoka kampuni 34 waliopewa kazi na Serikali ya kusambaza umeme katika vijiji vyote ambavyo bado havina umeme kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu mzunguko wa Pili (REA III, Round II) na kuwaagiza kwenda kwenye maeneo yao ya kazi.

Kikao kazi hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Naibu Katibu Mkuu, Kheri Mahimbali, Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Edward Ishengoma, Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Nishati, Mhandisi Styden Rwebangila, Watendaji Wakuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na wasimamizi wa miradi ya REA kutoka Wizara ya Nishati, TANESCO na REA.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wakandarasi wa mradi wa usambazaji umeme Vijijini wa Awamu ya Tatu, mzunguko wa Pili (hawapo pichani). Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato.

“Tunataka wakandarasi muwe kwenye maeneo yenu ya kazi, na wale wakandarasi kutoka nje ya nchi muwe na ofisi zenu hapa nchini, hatuwezi tukawapa ninyi kazi na mnaachia vibarua tu kuwa kwenye maeneo ya kazi na wakati hawana mamlaka, nyie wakurugenzi pia muende pia kwenye maeneo ya kazi.” Amesema Dkt.Kalemani.

Waziri wa Nishati ametumia kikao kazi hicho kuwapa maelekezo mahsusi wakandarasi hao ili mradi huo uweze kufanyika kwa ufanisi ikiwemo kuwataka kufanya kazi kwa kasi, ubunifu na usahihi wenye weledi pamoja na masharti mengine yaliyo kwenye mikataba yao.

Kuhusu kufanya kazi kwa kasi, amesema kuwa wakandarasi hao wanapaswa kufanya kazi na kumaliza ndani ya muda, ambao ni miezi 18 au kabla ya hapo.

Baadhi ya Mameneja wa TANESCO kutoka sehemu mbalimbali nchini pamoja na Wakandarasi wa mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu, mzunguko wa Pili wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani (hayupo pichani) wakati alipofanya kikao na wakandarasi hao jijini Dodoma.

Katika suala la ubunifu, amewataka wakandarasi hao kukidhi mahitaji ya wananchi kwani wanachohitaji wananchi hao ni umeme na sio kuona tu miundombinu inapita.

Vilevile kuhusu usahihi, amesema kuwa Serikali inategemea kuona thamani ya pesa inayotumika kwenye mradi huo na ishara mojawapo ni umeme kuunganishwa kwa wananchi wengi na Taasisi na Taasisi za umma.

Dkt.Kalemani ameagiza pia, kila mkandarasi anapofika kwenye eneo lake la kazi atoe taarifa kwa uongozi wa eneo husika ikiwemo Wakuu wa Wilaya na Wawakilishi wa wananchi jambo litakalopelekea kuwa na ushirikiano na kazi zao kufanyika kwa ufanisi.

Waziri wa Nishati pia ameagiza vifaa vya kazi vitakavyotumika kwenye mradi huo viwe bora na isitokee wananchi wanawashiwa umeme leo halafu kesho vifaa kama vile transfoma vinaharibika.

Pia, ametoa agizo, vifaa vinavyopatikana ndani ya nchi ndivyo vitumike kama kwenye mradi huo wa REA III mzunguko wa Pili ikiwemo nyaya, transfoma na nguzo ili kurahisha kazi na kutoa ajira kwa wananchi.

Vilevile, ameelekeza wakandarasi kuweka magenge mengi ya kazi na yasipungue matano kwenye kila eneo wanalofanyia kazi na pia watumie vijana wanaotoka katika maeneo wanayofanyia kazi

Suala la kuwacheleweshea umeme wananchi waliolipia huduma ya umeme, ameelekeza kuwa lisieendelee na wananchi waunganishiwe umeme ndani ya siku 14 baada ya kufanya malipo.

Dkt.Kalemani pia amewaelekeza TANESCO na REA kuwasimamia wakandarasi na kuwakagua muda wote, kuwawekea mazingira wezeshi ya kufanya kazi zao na kuchukua hatua kwa mujibu wa mikataba.

Waziri wa Nishati pia ameelekeza kuwa,wakandarasi lazima wawe na maeneo ya kuweka vifaa vya kazi, wasiuzie nguzo wananchi na wakandarasi wanaotandaza nyaya za umeme kwenye nyumba za wananchi, lazima wajulikane na REA, TANESCO nawakandarasi waliopewa kazi ya kusambaza umeme kwenye vijiji ili kuepusha wananchi kutapeliwa, kufanyiwa kazi chini ya viwango, na kupewa gharama zisizo stahiki.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato amesema kuwa, atahakikisha lengo na adhma ya Serikali ya kuwa, ifikapo mwaka 2022 kila kijiji nchini kinapata umeme linafikiwa na kwamba maelekezo aliyoyatoa Waziri wa Nishati ni mahsusi na yanapaswa kufanyiwa kazi ili kufikia lengo tajwa.

Amesisitiza pia kuhusu wakandarasi kutoa taarifa kwa wawakilishi wa wananchi na viongozi mbalimbali mara wanapokuwa katika maeneo ya kazi.

Aidha, ameagiza kuwa, Wakandarasi waweke utaratibu wa wananchi kulipia kidogo kidogo gharama za kuunganisha umeme vijijini ili waweze kupata huduma hiyo kwani wengine hawana uwezo wa kulipa shilingi 27,000 kwa mkupuo, akitoa mfano kuwa, fedha hizo zinaweza kulipwa ndani ya mwezi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali amesema kuwa, Wizara imepokea maelekezo yaliyotolewa kwenye kikao hicho na itayasimamia.