WANAFUNZI CHUO CHA MIPANGO WAJIFUNZA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA NISHATI NCHINI.
Wanafunzi wa Chuo cha Mipango Dodoma (IRDP), wamepata fursa ya kujifunza utekelezaji na usimamizi wa miradi ya Nishati inayotekelezwa nchini chini ya usimamizi wa Wizara ya Nishati.
Wanafunzi hao kutoka kozi ya Mipango na Usimamizi wa Miradi (Project Planning and Management) walipata elimu hiyo baada ya kutembelea Banda la Wizara ya Nishati katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 katika viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma, Juni 21, 2026.
Mmoja wa Wanafunzi hao Diana Samuel alisema kuwa lengo la kutembelea banda la wizara ni kujifunza kwa vitendo na kupata uelewa kwa kina kuhusu miradi mbalimbali inayotekelezwa na kusimamiwa katika sekta ya nishati nchini.
Wakiwa katika banda hilo, wanafunzi hao walipata fursa ya kuhoji na kujadiliana na wataalam kuhusu miradi inayosimamiwa na Taasisi zilizo chini ya Wizara ikiwepo miradi ya Mafuta na Gesi Asilia inayotekelezwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Pia walijifunza namna ambavyo taasisi zinapanga maeneo ya utekelezaji wa Miradi na usimamizi wake.
Aidha walifahamishwa namna ya kutambua, kutathmini na kudhibiti hatari mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa miradi mikubwa ili kuhakikisha malengo yanayowekwa yanafikiwa kwa ufanisi.
Wanafunzi hao pia walielezwa kuhusu majukumu ya Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), ikiwemo nafasi yake katika kuratibu uagizaji wa mafuta nchini, wataalamu walifafanua mbinu na mifumo inayotumika kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za mafuta nchini wakati wote.
Vilevile, wanafunzi hao walipata maelezo kuhusu Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), unaozalisha umeme megawati 2115 na mchango wake katika kuongeza upatikanaji wa umeme nchini.
Kwa upande wa Nishati Safi ya Kupikia, wanafunzi hao walielezwa mikakati ya Serikali kuhakikisha wananchi wanahamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutoa elimu sahihi na ruzuku kwa majiko banifu na mitungi ya gesi.
Pia walielezwa kuwa Serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu faida za matumizi ya nishati safi ya kupikia, hatua inayolenga kuboresha afya, kulinda mazingira na kufikia malengo ya kitaifa ya kuhakikisha ifikapo 2034 asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.