The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

WANAFUNZI WA UHANDISI WA PETRO...

WANAFUNZI WA UHANDISI WA PETROLI NA GESI UDOM WAPATA ELIMU YA KINA KUHUSU FURSA ZA SEKTA YA NISHATI.

Wanafunzi wa Shahada ya Uhandisi wa Petroli na Gesi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) walitembelea banda la Wizara ya Nishati katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yaliyofanyika katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma, kwa lengo la kujifunza na kupata uelewa wa kina kuhusu shughuli, miradi na fursa mbalimbali zinazoratibiwa na kusimamiwa na Wizara katika sekta ya nishati.

Katika ziara hiyo, wanafunzi hao walipatiwa elimu kuhusu maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi asilia nchini, utekelezaji wa miradi ya nishati, matumizi ya nishati safi ya kupikia, pamoja na fursa zinazopatikana kwa vijana kushiriki katika ukuaji na maendeleo ya sekta hiyo. Aidha, walipata nafasi ya kujionea utekelezaji wa sera na mipango mbalimbali ya Serikali inayolenga kuimarisha upatikanaji wa nishati kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Ziara hiyo imewasaidia kuunganisha maarifa wanayopata darasani na hali halisi ya utekelezaji wa miradi ya nishati nchini, huku ikiwapa hamasa ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa Taifa.

Wizara ya Nishati iliendelea kuwakaribisha wananchi, wanafunzi wa shule na vyuo, pamoja na wadau mbalimbali kutembelea banda lake ili kupata elimu kuhusu huduma za nishati, miradi inayotekelezwa nchini, matumizi ya nishati safi ya kupikia na fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta ya nishati.