Wananchi Nkasi waiomba Serikali nishati safi na salama ya kupikia
Wananchi Nkasi waiomba Serikali nishati safi na salama ya kupikia
Wananchi mbalimbali katika Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa wameiomba Serikali kuwapatia nishati safi na salama ya kupikia ili waweze kufanya shughuli za kuwaingizia kipato ikiwemo ukaangaji wa samaki na dagaa bila kuathiri afya zao kutokana na moshi.
Maombi hayo yalitolewa kwa nyakati tofauti wakati Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba alipofanya ziara katika Kijiji cha Kilando na Kisiwa cha Mandakelenge wilayani Nkasi ili kusikiliza kero za wananchi, kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kukagua usambazaji umeme katika Kisiwa cha Mandakelenge ambacho kinapata umeme baada ya Serikali kupitisha nyaya za umeme chini ya maji katika Ziwa Tanganyika .
Mmoja wa wananchihao,Bw. Gerald Muta Kutoka Kisiwa cha Mandakelenge, pamoja na kushukuru Serikali kuwapelekea umeme kwenye Kisiwa hicho, alimwomba Waziri wa Nishati kuwawezesha kinamama wajasiriamali kupata nishati safi ya kupikia ili wafanye kazi ya kukaanga samaki na dagaa kwa wingi kwani kisiwa hicho kwa sasa kina uhaba wa kuni na mkaa.
Mbele ya Waziri wa Nishati, Bi.Zurietha Msarange kutoka Kisiwa cha Mandakelenge alisema, “Tunakuomba Mhe Waziri utuwekee miundombinu ya kisasa ya kupikia ili tuweze kufanya biashara ya samaki na kuuza maeneo mengine hali itakayotuongezea kipato.”
Akizungumza na Wananchi katika kisiwa hicho Waziri wa Nishati alisema kuwa,upatikanaji wa kuni na mkaa ni changamoto kwenye Visiwa kwani unaweza kusababisha visiwa hivyo kuwa jangwa na kwamba maeneo kama hayo yanapaswa kuwa mfano wa matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.
Katika kutekeleza mpango wa Serikali wa upatikanaji wa nishati safi na salama ya kupikia, Waziri wa Nishati alitoa mitungi 50 kwa vikundi mbalimbali vya kina mamalishe na kueleza kuwa huo ni mwanzo wa safari ya kufikia mahala ambapo kila nyumba nchini itatumia nishati safi ya kupikia isiyotoa moshi ambao una athari kwa afya.
Awali akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Kilando wilayani Nkasi, Waziri Makamba alieleza kuhusu kazi za usambazaji umeme zinazoendelea katika Mkoa wa Rukwa ambao una vijiji 339 na tayari vijiji 199 vimeshasambaziwa umeme na kuahidi kuwa vijiji vyote vilivyosalia vitasambaziwa umeme kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili.
Aidha aliwaeleza wananchi juhudi zinazochukuliwa na Serikali ili kuwa na unafuu katika bei ya mafuta hali inayoifanya Tanzania kuwa nchi inayouza mafuta kwa gharama nafuu ukilinganisha na bei katika nchi zinazoizunguka.
“Tunamshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwani bila ruzuku ya shilingi Bilioni 100 anayoitoa kila mwezi bei ya Mafuta ingekuwa imeongezeka sh.500 kwa kila lita ya Dizeli na sh.200 kwa kila lita ya Petroli.” Alisema Waziri Makamba.