WATANZANIA WAASWA KUBADILI MTINDO WA MATUMIZI YA GESI ASILIA KATIKA USAFIRI NA UPISHI.
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amewataka Watanzania kubadilika kimtazamo na kuanza kutumia gesi asilia katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi, ikiwemo usafiri na upishi, badala ya kutegemea zaidi nishati ya mafuta.
Mhe. Salome ametoa rai hiyo, Novemba 13, 2026, alipotembelea Kituo cha Kuchakata Gesi Asilia cha Madimba kilichopo mkoani Mtwara.
Amesema upanuzi wa kituo hicho utafungua fursa zaidi za matumizi ya gesi asilia katika vyombo vya usafiri pamoja na matumizi ya kupikia majumbani, hatua ambayo ni habari njema kwa sekta ya nishati na uchumi wa wananchi.
Ameeleza kuwa matumizi ya gesi asilia yanatoa fursa ya kujenga uchumi unaotumia nishati kwa gharama nafuu, hivyo kupunguza gharama za maisha na kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji.
Aidha, amesisitiza kuwa ni wakati sasa kwa Watanzania kunufaika na rasilimali ya gesi asilia iliyopo nchini kwa kuachana na utegemezi wa kuni na mkaa na kuelekea kwenye matumizi ya gesi katika kupikia majumbani.
Vilevile, amewahimiza wananchi na wadau wa sekta ya usafiri kuanza kutumia gesi asilia katika magari, pikipiki na bajaji ili kupunguza utegemezi wa mafuta ya petroli na dizeli.
Ameongeza kuwa Serikali imeweka ruzuku kubwa katika vifaa vinavyohitajika kwa matumizi ya gesi asilia, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwezesha wananchi kupata na kutumia nishati hiyo kwa urahisi.