The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

WATENGENEZA MAUDHUI WAHAMASISH...

WATENGENEZA MAUDHUI WAHAMASISHWA KUTUMIA FURSA ZA NISHATI SAFI YA KUPIKIA KUELIMISHA JAMII NA KUJIPATIA KIPATO.

Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia, Nolasco Mlay, amewahimiza watengeneza maudhui nchini kutumia ubunifu wao kuelimisha jamii kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, huku wakitumia fursa hiyo kujiongezea kipato.

Ameyabainishahayo Machi 25, 2026, jijini Dar es Salaam wakati akizungumza kwenye mafunzo kwa watengeneza maudhui (content creators), yaliyoandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania, huku Wizara ya Nishati ikiwa miongoni mwa wawezeshaji wakuu.

Akizungumza katika mafunzo hayo ameeleza kuwa Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, angalau asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ambapo amebainisha kuwa suluhisho za nishati safi ya kupikiazipo na zinaendelea kuwafikia wananchi, kilichobaki ni kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia watu wengi zaidi ili kuchochea mabadiliko ya matumizi.

Amesema licha ya hatua iliyofikiwa, bado kuna changamoto ya uelewa mdogo kwa wananchi kuhusu nishati safi ya kupikia, ambapo wengi hudhani kuwa ni matumizi ya gesi pekee. hivyo amefafanua kuwa nishati safi ya kupikia inajumuisha pia matumizi ya umeme, gesi asilia, biyogasi, mkaa mbadala na teknolojia nyingine mbadala ambazo husaidia kupunguza athari za kiafya na kimazingira.

Bw. Mlay amesisitiza kuwa watengeneza maudhui wana nafasi kubwa ya kubadilisha mtazamo wa jamii kwa kutengeneza video za elimu, vichekesho, hadithi na kampeni mbalimbali zitakazowafikia wananchi kwa urahisi ambapo amesisitiza kuwa maudhui hayo yakifanyika kwa ubunifu na ubora, yanaweza kununuliwa na kuwapatia kipato watayarishaji wake huku yakisaidia kusambaza ujumbe muhimu kwa jamii.

Ametoa wito kwa watengeneza maudhui hao kuchangamkia fursa hiyo kwa kuandaa kazi zenye kuelimisha kuhusu faida za nishati safi ya kupikia pamoja na madhara ya kutumia nishati zisizo safi, akisisitiza kuwa jamii ikipata taarifa sahihi, itafanya mabadiliko chanya yatakayoboreshwa maisha na kulinda afya za Watanzania.