The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

WATUMISHI WIZARA YA MAMBO YA N...

WATUMISHI WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI WAPATIWA ELIMU YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA.

Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wamepatiwa elimu kuhusu matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kupitia mafunzo yaliyotolewa na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati.

Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kufikia lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Mafunzo hayo yaliwashirikisha watumishi kutoka idara na vitengo mbalimbali vya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambapo wamepata uelewa kuhusu aina za nishati safi za kupikia, faida za matumizi ya nishati safi ya kupikia katika kulinda afya, mazingira na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Akizungumza baada ya mafunzo hayo, Afisa Dawati kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bi. Ester Kitachang’wa, alipongeza Wizara ya Nishati kwa kutoa elimu hiyo muhimu na kueleza kuwa washiriki wamejifunza mambo mengi yatakayowasaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Aidha, Bi. Kitachang’wa alisema, mafunzo hayo yatawasaidia kuwa mabalozi wazuri wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa watumishi wenzao ambao hawakupata bahati ya kuhudhuria mafunzo hayo na jamii kwa ujumla ili kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi.