Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​Wawekezaji kutoka Uganda waon...

​Wawekezaji kutoka Uganda waonyesha nia ya kuwekeza katika miradi ya umeme Tanzania

Wawekezaji kutoka Uganda waonyesha nia ya kuwekeza katika miradi ya umeme Tanzania

Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uganda nchini Tanzania pamoja na wawekezaji kutoka nchini humo wamemweleza Waziri nia yao ya kuwekeza katika miradi mbalimbali ya umeme ukiwemo wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Lindi, Masasi, Tunduru na Songea.

Mazungumzo hayo yalifanyika Machi 21, 2023 katika ofisi za Wizara ya Nishati jijini Dodoma na kuwashirikisha Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka, Kamishna Msaidizi Maendeleo ya umeme, Mhandisi Styden Rwebangila na wawekezaji kutoka Uganda.

Wawekezaji hao walimueleza Makamba kuwa wanataka kuwekeza katika mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa Msongo mkubwa wa Kilovolti 400 wenye urefu wa Kilometa 222.3 kutoka Lindi, Masasi hadi Songea.

Wamesema kuwa watawekeza katika kusanifu, kutafuta fedha, kujenga na kuendesha njia hiyo na kuikabidhi baada ya muda uliopangwa wataikabidhi njia hiyo kwa TANESCO.

Waziri Makamba pamoja na kueleza kuwa, Serikali inawakaribisha wawekezaji kama hao, amewaagiza kukutana na Shirika la Umeme nchini na maafisa wa Wizara ya Nishati ili kujadiliana na kuona njia bora ya kutekeleza mradi huo kwa kuangalia sheria, taratibu na kanuni za uwekezaji katika miradi ya umeme.

Aidha Wawekezaji hao pia wameonyesha nia ya kutaka kuwekeza katika mradi wa umeme wa jua katika Kisiwa cha Mafia wenye megawati 5.

Hata hivyo Waziri aliwaeleza wawekazaji hao kuwa serikali imeshapata kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 5 kutoka Wakala wa Maendeleo wa Ufaransa (AFD) na kwamba iko katika mazungumzo ya AFD kuongeza fedha zaidi za kutekeleza mradi huo.

Kwa upande wake Balozi wa Uganda nchini Tanzani, Col. Mwesigye Fred ameishukuru Serikali ya Tanzania, kwa kukubali wawekezaji kutoka nchi Uganda kuwekeza katika miradi ya umeme.

Amesema hayo ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya nchi hizo mbili ulioasisiwa na viongozi wakuu.