WAZIRI HOMERA AKUTANA NA UONGOZI WA TANESCO, ATOA MAELEKEZO KUJIANDAA KUKABILIANA NA EL NINO.
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amekutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ikiwa ni sehemu ya kujitambulisha na kufahamiana na uongozi wa Shirika pamoja na kupata taarifa kuhusu maandalizi ya TANESCO kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Nino.
Kikao hicho kimefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam, ambapo Waziri Homera amepokea taarifa kuhusu mikakati na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na TANESCO kuhakikisha mfumo wa umeme unaendelea kuwa salama na huduma ya umeme inapatikana kwa uhakika nchini.
Aidha, kikao hicho kimejadili maandalizi ya TANESCO katika kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo, ikiwemo ulinzi wa miundombinu ya umeme, utayari wa timu za kiufundi na hatua za haraka za kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza, kwa lengo la kuhakikisha wananchi na watumiaji wengine wa umeme hawaathiriki.
Katika kikao hicho, Waziri Homera amesisitiza umuhimu wa TANESCO kuwa na utayari wa kutosha na kuchukua hatua za mapema ili kulinda miundombinu ya umeme na kuhakikisha huduma inaendelea kutolewa kwa uhakika.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Ndg. Lazaro Twange, pamoja na Menejimenti ya Shirika.