Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

WAZIRI MAKAMBA ATATUA CHANGAMO...

WAZIRI MAKAMBA ATATUA CHANGAMOTO YA UMEME SENGEREMA

Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba ametatua changamoto ya muda mrefu ya kutopata umeme wa uhakika wilayani Sengerema kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukatika kwa laini iliyokuwa ikipeleka umeme wilayani humo kutokea Mwanza ambako kulisababishwa na shughuli za ujenzi wa Daraja la Busisi na kupelekea umeme kukatika zaidi ya mara 10 kwa siku.

Waziri wa Nishati alitatua changamoto hiyo tarehe 14 Julai, 2022 baada ya kufika wilayani humo ikiwa ni sehemu ya ziara yake siku 21 katika mikoa 14 nchini ambapo pamoja na kukagua miradi inayotekelezwa na Wizara ya Nishati kupitia Taasisi zake, ziara hiyo imelenga kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua.

“Sababu za kutokuwa na umeme wa uhakika wilayani hapa ni uchakavu wa miundombinu na kukua kwa mahitaji, lakini sisi pia hatukufanya kazi ya kupanua na kuboresha miundombinu ili kuendana na mahitaji ya sasa. Awali, Sengerema ilikuwa ikipata umeme kutoka njia ya Geita na Mwanza lakini njia ya mwanza ilikatika kwa bahati mbaya, hivyo kufanya Sengerema kupata umeme kutokea Geita pekee ambao hautoshi.” Alisema Makamba

Ili kutatua changamoto hiyo, Waziri Makamba alisema kuwa, hadi kufikia mwezi wa 10 mwaka huu itajengwa njia nyingine ya umeme kutokea kituo cha Mpomvu Geita ambayo itapeleka umeme wa megawati 20 wilayani humo na hivyo kukidhi mahitaji kwani kwa sasa matumizi ya umeme ya Sengerema ni megawati 5 hadi 6.

Aliongeza kuwa, Daraja la Busisi litakapomalizika itajengwa tena laini ya umeme kutokea jijini Mwanza na hivyo kufanya Wilaya hiyo kuwa na uhakika zaidi wa upatikanaji umeme na kwamba kutakuwa na laini nyingine ya kV 220 ambayo itapita pia wilayani humo ambayo imelenga kupeleka umeme kwenye migodi.

Kuhusu umeme vijijini, alisema kuwa Wilaya hiyo ina vijiji 153 na tayari vijiji 143 vimeshasambaziwa umeme na kwamba Vijiji 10 vilivyobaki vinaendelea kusambaziwa umeme kupitia mradi wa umeme vijijini wa Awamu ya Tatu, mzunguko wa Pili.

Akiwa wilayani Sengerema, Waziri wa Nishati aligawa mitungi ya gesi takriban 80ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo alifafanua kuwa, hiyo ni programu maalumu ya majaribio ambayo itawezesha upatikanaji wa taarifa zitakazozewesha kutengeneza mpango mkubwa wa kitaifa wa usambazaji wa gesi nchini na kwamba programu hiyo ni ya miezi Sita na wanufaika ni kinamama.

Kuhusu usambazaji umeme visiwani, alisema kuwa shilingi bilioni 54 zimetengwa kwa ajili ya kusambaza umeme kwenye visiwa takriban 47 nchini huku visiwa 35 vikiwa ndani ya Ziwa Victoria.

Waziri wa Nishati, pia aliwasha umeme katika shule ya watoto wenye mahitaji maalum ya Kizugwangoma ambapo Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Benedicto Bijiga alimweleza Waziri kuwa, umeme huo sasa unawawezesha wanafunzi hao wenye mahitaji maalum kujifunza kwa kutumia luninga, kupata burudani na pia kurahisisha matumizi mengine kama ya kuchapa na kudurufu mitihani.