WAZIRI NDEJEMBI AONGOZA KIKAO KAZI NA VIONGOZI WA TANESCO
Waziri Wizara ya Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameongoza kikao kazi cha Watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Jijini Dodoma.
Mhe. Ndejembi ameeleza kuwa lengo la kikao kazi hicho ni kujadili utekelezaji wa majukumu ya Shirika, kupanga mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja, lakini pia kufanya tathmini ya utendaji kazi na kuweka mikakati mipya ili kuongeza kasi ya utoaji huduma bora.
Naye, Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Bw. Lazaro Twange ameeleza kuwa wao kama shirika wanahusika na Uzalishaji wa Umeme, Usafirishaji wa Umeme pamoja na Usambazaji wa Umeme kwa wateja. Ameleeza kuwa, kwasasa kuna miradi 41 inayofadhiliwa na Serikali ya Tanzania lakini pia Wahisani wa Maendeleo, na kupelekea kuwa Jumla ya gharama za miradi hiyo ni takriban ya trilioni 13.4
Sambamba na hilo Shirika la Umeme Tanzania linamiliki Uwezo wa MW 3,807.69 sawa na asilimia 93.47 huku Makampuni binafsi yakiwa na MW 266.01 sawa na asilimia 6.53.
‘’Sisi kama Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) tumejipanga ndani ya siku mia moja kutekeleza miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufunga Transfomer mpya 500, lakini pia ufungaji wa mita Janja (Smart meter) 200,000 kwa wateja’’. Ameeleza Twange.
Naye, Balozi Zuhura Bundala Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) amemshukuru sana Waziri wa Nishati Mhe. Deogratius Ndejembi kwa kuhudhuria kikao kazi hicho amesema.
"Sisi kama bodi tunakuhakikishia kuwa shirika lina watalaam wakutosha na kwa kipindi ambacho tumefanya nao kazi, kumekuwa na Maamuzi mbalimbali ambayo sisi kama Bodi tumesimamia na kutekeleza na kumekuwa na mafanikio makubwa sana.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mha. Felchesmi Mramba amemshukuru sana Waziri wa Nishati Mhe. Deogratius Ndejembi kwa kufanya kikao kazi hicho na Watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO, Mha. Mramba amesema.
“Nalipongeza sana Shirika hili kwani linafanya kazi kubwa sana ya kupeleka huduma bora kwa wananchi” amesema Mha. Mramba.
Naye, Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Salome Makamba amesema kikao hiki ni muhimu kwasababu tunaona dhamira yako Mhe. Waziri wa Nishati ya dhati ya kupeleka huduma bora kwa wananchi wa Tanzania hususani yale maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hii.
