WAZIRI NDEJEMBI AZINDUA MKAKATI MPYA WA MAGEUZI YA NISHATI AFRIKA.
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi amezindua Mkakati na Mpango Kazi wa Mageuzi ya Nishati kwa Bara la Afrika, ambao utaanza kutekelezwa kupitia Kamisheni ya Nishati ya Afrika (AFREC) ili kuongeza upatikanaji wa nishati na kuharakisha mabadiliko ya matumizi ya nishati safi.
Uzinduzi huo umefanyika Disemba 11, 2025 Jijini Addis Ababa, Ethiopia, ikiwa ni sehemu ya Kongamano la Nishati la Umoja wa Afrika (AU Energy Summit) ambalo limehudhuriwa na Mawaziri wa Nishati, Wadau wa Sekta ya Nishati, na Washirika wa Maendeleo kutoka nchi mbalimbali Barani Afrika.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Ndejembi amesisitiza umuhimu wa Bara la Afrika kuwekeza kikamilifu katika nishati safi na mbadala ili kupunguza utoaji wa hewa ukaa ambao kwa sasa unakadiriwa kuchangia asilimia 4 ya hewa chafu duniani.
Amesema matumizi ya nishati safi katika viwanda, majumbani, sekta ya usafiri na majengo ni hatua muhimu katika kulinda mazingira na kuimarisha uchumi.
Ameongeza kuwa ili kufanikisha mkakati huo, nchi za Afrika zinapaswa kutumia vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme kama vile jua, upepo, maji, gesi asilia na vyanzo vingine vinavyopatikana kwa wingi barani humo. Hii ni kwa ajili ya kufikia lengo la kupeleka huduma ya umeme kwa watu milioni 600 ambao bado hawajafikiwa.
“Tukiwa kama viongozi wa Afrika tunalo jukumu la kuhakikisha watu wetu wote wanapata huduma ya umeme wa uhakika. Kupitia mkakati wa ‘Mission 300’ Tanzania imejipanga kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 watanzania wote wanapata umeme, na hadi sasa tumevuka hatua kubwa kwa kufikia asilimia 85” amesema Mhe. Ndejembi.
Katika kongamano hilo, Mhe. Ndejembi aliambatana na Kamishna wa Nishati wa Wizara ya Nishati, Mhandisi.Innocent Luoga, ambaye pia ameshiriki katika majadiliano ya kitaalam kuhusu utekelezaji wa mageuzi ya nishati barani Afrika.
