Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

Wizara ya Fedha yaridhishwa na...

Wizara ya Fedha yaridhishwa na maboresho ya Kituo cha umeme Zuzu

Wizara ya Fedha yaridhishwa na maboresho ya Kituo cha umeme Zuzu

Wizara ya Fedha na Mipango imeeleza kuridhishwa kwake na maboresho yanayoendelea kufanyika katika Kituo cha Umeme cha Zuzu mkoani Dodoma ambacho kimeongezewa uwezo kutoka megawati 48 hadi megawati 648.

Hayo yalibainishwa tarehe 26 Julai, 2021 wakati wa ziara Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Fedha na Mipango walioongozwa na Kamishna wa Fedha za Nje, Sauda Msemo ambaye alimwakilisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.

Kituo hicho, ambacho awali kilikuwa na uwezo wa megawati 48 kwa sasa kimeongezewa transfoma ambazo kwa ujumla zinafanya kituo hicho kuwa na uwezo wa megawati 648 na hivyo kupelekea umeme mkoani Dodoma kuwa uhakika na kuongezeka kwa laini zinazopeleka umeme katika maeneo mbalimbali.

“Tumekuja kuangalia kituo hiki cha Zuzu ili kuona hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi huu, na kuelewa kazi zilizobaki ili kukamilisha mradi na kama kuna changamoto zinazohitaji kutatuliwa ili kuweza kukamilisha mradi ili kupata matokeo yaliyotarajiwa.” Amesema Msemo

Alisema kuwa, Wizara hiyo imeridhishwa na hatua iliyofikiwa hadi sasa na pia mikakati iliyowekwa ili kukamilisha mradi huo na kwamba Wizara ya Fedha na Uchumi imekuwa ikishirikiana na Wizara ya Nishati katika utekelezaji wa miradi mbalimbali na imekuwa ikitoa fedha kwa wakati kutekeleza miradi ya Nishati.

Aliongeza kuwa, katika ziara hiyo wamepata uelewa wa masuala mbalimbali ikiwemo umuhimu wa uwepo wa vituo vya uzalishaji umeme katika maeneo mbalimbali nchini ili kuweza kuwa na uhakika wa uwepo wa umeme na usalama wake.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali alisema kuwa, ziara hiyo imekamilisha ziara ya viongozi hao katika miradi mbalimbali ya Nishati iliyoanzia katika mradi wa umeme wa Julius Nyerere, na kwamba Wizara ya Fedha na Mipango ni wadau muhimu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Nishati hivyo ziara hiyo imesadia kupata uelewa wa pamoja utakaorahisisha majadiliano na maamuzi yanayofanyika.

Alitoa wito kwa wadau wengine kutembelea miradi ya nishati ili kujenga uelewa wa pamoja utakaosaidia kusukuma mbele gurudumu la maendeleo kwani nishati ndiyo injini ya ukuaji wa uchumi.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi, Mhandisi Peter Kigadye alisema kuwa upanuzi wa kituo umehusisha kuongeza uwezo kituo kwenda kV 220 na sasa kinaongezewa uwezo wa kV 400 ambao kwa ujumla kufanya kituo hicho kuwa na uwezo wa megawati takriban 648.

Aliongeza kuwa, kituo hicho pia kitapokea umeme kutoka mradi wa umeme wa Julius Nyerere na kupeleka maeneo ya mbalimbali ya nchi. Mradi wa upanuzi wa Kituo cha Zuzu unatarajiwa kukamilika rasmi mwezi Septemba mwaka huu.