Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

Wizara ya Nishati yatoa lita 1...

Wizara ya Nishati yatoa lita 14,500 za Petroli na Diseli huko Katesh

Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga, kwa Niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Doto Biteko amesema Wizara ya Nishati imetoa Mafuta Lita 14,500 ya Petroli na Dizeli kwa ajili ya kusaidia na kurahisisha shughuli zinazoendelea katika Mji wa Katesh uliokubwa na janga la Maporomoko ya Udongo wilayani Hanang Mkoani Manyara.

Mhe. Kapinga amesema hayo, tarehe 7 Desemba, 2023 baada ya kuwasili katika eneo hilo ili kuona uharibifu wa Miundombinu ya Sekta anayoisimamia ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Magizo la Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyatoa kwa Viongozi wote.

Mafuta ya Petroli pamoja na Dizeli yaliotolewa ni kwa ajili ya Mitambo na Magari yanayotumika katika kuondoa matope na magogo katika eneo hilo.

Amesema Mafuta hayo yametolewa na Umoja Makampuni ya Uagizaji Mafuta Tanzania (TAOMAC) pamoja na Wadau mbalimbali wanaohusika na Sekta hiyo.

Ameomba Makampuni hayo na Wadau wengine wanaohusika na Sekta ya Nishati kuendelea kutoa michango muhimu kwa wananchi hao katika eneo hilo.

Kuhusu Nishati ya Umeme , Mhe. Kapinga amesema tayari huduma ya Umeme imerejea katika hali yake ya kawaida na zoezi linaloendelea sasa kuunganisha nyumba zilizopata changamoto.

Mashineumba 76, Nguzo 60 pamoja na Njia ya kusafirisha umeme wa Msongo Mdogo ziliathiriwa na Maporomoko hayo.

Katika zoezi hilo Naibu Waziri ameambatana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka na Viongozi Waandamizi kutoka Shirika na Umeme Tanzania (TANESCO)

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini(GPSA), Charles Mtiesa amekiri kupokea mafuta hayo kwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Mkoa wa Manyara na kusema kuwa watayasimamia na kuhakikisha mafuta hayo yanatumika kwa shughuli iliyokusudiwa.