ZAMBIA YAVUTIWA NA MFUMO WA TANZANIA WA USAMBAZAJI UMEME VIJIJINI NA NISHATI SAFI YA KUPIKIA.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati nchini Zambia, Mhandisi Arnold Simwaba, amesema nchi yake imevutiwa na mfumo wa Tanzania wa kusambaza umeme vijijini na matumizi ya nishati safi ya kupikia unaoratibiwa chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Akizungumza wakati wa ziara ya watendaji wa REA- Zambia nchini Tanzania Simwaba amesema nchi hiyo inategemea zaidi Wizara ya Nishati na sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini na nishati safi ya kupikia lakini Tanzania imefanikiwa zaidi kupitia uratibu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Amesema ziara hiyo imewapa mwelekeo mpya wa namna ya kuboresha mfumo wa usambazaji wa nishati nchini Zambia, huku akisisitiza umuhimu wa nchi jirani kujifunza kutoka kwa kila mmoja ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Aidha, Mha. Simwaba amesema ushirikiano wa sekta ya nishati kati ya Tanzania na Zambia unafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya kiuchumi, hasa kupitia utekelezaji wa miradi ya pamoja ya kimkakati ikiwemo bomba la mafuta la TAZAMA na mradi wa kuunganisha mifumo ya umeme wa kikanda wa TAZA.
Ujumbe wa Wizara ya Nishati kutoka nchini Zambia ulihitimisha ziara ya mafunzo jijini Dodoma Juni 25, 2026, ikiwa na lengo la kujifunza mikakati ya Tanzania katika kusambaza umeme vijijini na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuharakisha lengo la Zambia la kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za nishati.