AFRIKA YATAKIWA KUUNGANA KUHAKIKISHA UPATIKANAJI WA NISHATI YA UHAKIKA.
Waziri wa Nishati wa Ghana, John Jinapor, amesema umefika wakati kwa nchi za Afrika kukaa pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya kuendeleza upatikanaji wa nishati ya uhakika na kuchochea maendeleo ya bara hilo.
Akizungumza katika siku ya kwanza ya Mkutano wa Wiki ya Mafuta Barani Afrika, unaofanyika Accra, Ghana, Jinapor amesema pamoja na mabadiliko ya nishati yanayoendelea duniani na barani Afrika, suala la upatikanaji wa nishati ya uhakika bado ni changamoto kubwa na linahitaji hatua za pamoja.
Amesema nchi za Afrika zinapaswa kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji, kuimarisha ushindani katika soko la nishati na kuhakikisha shughuli za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi zinaendelea ili kukidhi mahitaji ya nishati katika bara hilo.
Kwa upande wa Tanzania, Mjiolojia Mkuu kutoka Wizara ya Nishati, Mussa Mussa, amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi na ya uwazi kwa wawekezaji katika sekta ya mafuta na gesi, kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2015.
Amesema sera hiyo inatoa fursa kwa wawekezaji wa ndani kushiriki katika sekta hiyo, ikiwemo kupitia ushirikiano na kampuni zenye uwezo wa kifedha katika utekelezaji wa miradi ya mafuta na gesi.
Akizungumzia suala la uwazi katika mikataba ya mafuta na gesi, Mussa amesema Bunge limekuwa moja ya nguzo muhimu katika kuhakikisha mikataba inapitiwa na kuthibitishwa kwa kuzingatia vigezo na taratibu zilizowekwa.
Aidha, amesema Tanzania inaendelea kushiriki katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa ambayo ni sehemu ya nchi wanachama, yanayolenga kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika mikataba na shughuli za sekta ya mafuta na gesi.
Wiki ya Mafuta Barani Afrika imefanyika kwa mara ya pili jijini Accra, Ghana, na imewakutanisha Mawaziri wa Nishati na sekta husika, kampuni za mafuta na gesi, wadhibiti wa sekta ya nishati, wadau mbalimbali wa nishati barani Afrika pamoja na wataalamu na wanazuoni wa masuala ya mafuta na gesi.