UKUWAJI WA SEKTA YA MADINI WAONGEZA MAHITAJI YA UMEME MIGODINI –TWANGE.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ameeleza kwamba ukuaji wa sekta ya madini nchini unahitaji umeme wa kutosha na wa uhakika hii inatokana na kasi ya ukuaji wa sekta ya madini ambapo imeongeza mahitaji makubwa ya umeme wa uhakika kwa ajili ya kuendesha mitambo ya wachimbaji wakubwa, wa kati, na wadogo.
Ndg Twange ameyasema hayo wakati wa hafla ya utiaji Saini mkataba wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme mpomvu – GGM msongo wa 220KV na Kituo cha Kupoza Umeme kilichoko GGM, Geita iliyofanyika jijini Dodoma Septemba 3,2026.
Ndg Twange ameeleza kwamba Mgodi wa Geita Gold Mine (GGM) ni miongoni mwa wateja wakubwa, ambapo yeye pamoja na wateja wengine wanachangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa mapato ya TANESCO ameeleza kuwa tangu mwaka 2024, TANESCO ilianza kuwahudumia kwa umeme wa hadi 16MW, ila kutokana na kuongezeka kwa mitambo ya mgodi huo, mahitaji yameongezeka na kufanya miundombinu ya sasa kutotosheleza, hivyo kuhitaji mradi wa kumwezesha kukidhi mahitaji yake ya kiuzalishaji ya kila siku.
Ameeleza kwamba mradi huo utahusisha pia Kujenga njia kubwa ya umeme yenye msukumo wa kilovoti 220 kutoka kituo cha Ponge-Geita kwenda mgodi wa dhahabu wa Geita umbali wa km 6.65, pamoja na kituo cha kupoza umeme.
Ameeleza kwamba TANESCO ilitenga mradi huu kupitia mfumo wa "Corporate Project" na kupata kibali cha shilingi bilioni 228 kutoka Serikalini kupitia Wizara ya Fedha, ambapo utekelezaji wa Mikataba Kutokana na fedha hizo, miradi 42 imeandaliwa ambapo miradi 38 ya kusambaza umeme na miradi 4 ya njia kubwa za kusafirisha umeme.
Ndg Twange ameeleza kuwa Mzabuni aliyeshinda tenda ya ujenzi wa mradi huo ni kampuni ya Crotech Engineering Company Limited akishirikiana na kampuni kutoka China kwa thamani ya shilingi bilioni 63.9. na muda wa utekelezaji utakuwa Miezi 18 kuanzia tarehe ya utiaji saini wa mkataba.
Ndg Twange ameogeza kuwa TANESCO imeweka utaratibu wa wazi wa kuunganishia umeme wachimbaji ambapo mteja analipia 60% ya gharama za mradi na 40% iliyobaki inakatwa kidogo kidogo kupitia bili zao za umeme, na pia Meneja wa Wilaya wa TANESCO amewezeshwa kisheria kusaini mikataba ya miradi hadi ya shilingi milioni 800 bila kuhitaji kupanda ngazi za juu, ili kurahisisha na kuharakisha huduma kwa wachimbaji.
Amewaomba Viongozi wa Mkoa na Wilaya kuhamasisha wachimbaji kutumia fursa hii ili kupata umeme wa uhakika na wa gharama nafuu.