Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​DKT.BITEKO AFUNGUA MKUTANO WA...

​DKT.BITEKO AFUNGUA MKUTANO WA MWAKA WA KIUTENDAJI WA MAAFISA USTAWI WA JAMII NCHINI

DKT.BITEKO AFUNGUA MKUTANO WA MWAKA WA KIUTENDAJI WA MAAFISA USTAWI WA JAMII NCHINI

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amefungua mkutano wa mwaka wa kiutendaji wa Maafisa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara za Kisekta, Taasisi za umma pamoja na sekta binafsi zinazotoa huduma za Ustawi wa Jamii nchini na kutoa maelekezo mahsusi yatakayofanya sekta hiyo kuwa imara na kutoa huduma bora katika Taifa.

Dkt.Doto Biteko amefungua Mkutano huo tarehe 6 Septemba, 2023 jijini Dodoma ambapo mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, Naibu Waziri, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Deogratius Ndejembi, na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Mhe. Patrobas Katambi.

Akifungua Mkutano huo kwa niaba ya Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Mpango, Dkt.Biteko ametoa maagizo mbalimbali kwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Ofisi ya Rais TAMISEMI na wadau wengine ikiwemo ya kuhakikisha kuwa mchakato wa mapitio ya sheria ya mtoto na kanuni zake unakamilikaili kuhakikisha watoto wanapata ulinzi na malezi stahiki.

Amewaelekeza pia, wahakikishe mchakato sheria ya wataalamu wa ustawi wa jamii inakamilika ili kupanua wigo na kusimamia maadili wa utoaji wa huduma za ustawi wa jamii.

Aidha, Wakurugenzi wa Halmashauri wametakiwa kutenga fedha kwa ajili ya huduma za Ustawi wa Jamii kwa mujibu wa mwongozo wa mipango, bajeti na taarifa za Ustawi wa Jamii.

Vilevile, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma wametakiwa kuendelea kutoa ajira kwa maafisa Ustawi wa Jamii ili kusaidia kutoa huduma bora za Ustawi wa Jamii

Dkt. Biteko ameagiza pia kuimarishwakwa programu ya huduma ya afya ya akili na msaada wa kisaikolojia ili kupunguza athari na changamoto zinazotokea ndani ya familia na jamii.

Agizo jingine lililotolewa ni uwekaji wa mfumo madhubuti wa ufuatiliaji wa makao ya Watoto na Makazi ya wazee ili kuhakikisha malengo ya msingi ya kuanzishwa vituo hivyo yanafuatwa kikamilifu na hayaanzishwi kiholela;

Aidha, Wizara ya Maendeleo ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta pamoja na Wadau wa Maendeleo imetakiwa kufanya tafiti ili kupata taarifa sahihi na takwimu ili kuboresha huduma za Ustawi wa Jamii.

Pia, Wizara ya Afya imeagizwa kuunda kitengo Maalum kitakachoshughulikia uratibu wa huduma za ustawi wa Jamii kutokana na umuhimu wa wataalamu wa Ustawi wa Jamii katika huduma za afya.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, amesema, Serikali imeendelea kuipa kipaumbelesekta hiyo kwakuwa imekuwa kimbilio la wananchi wenye uhitaji wa huduma hiyo na kuwahakikishia kutoa ushirikiano muda wowote.

Aidha,amesema sekta ya ustawi wa jamii ikifanya kazi kwa weledi na ufanisi itapunguza mzigo kwa Serikali kwa kuwa changamoto za kijamii zitapungua na fedha ambazo zimetengwa zitatumika katika kuendeleza maendeleo mengine.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum; Dkt. Dorothy Gwajima, amewataka watumishi hao kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili huduma hiyo ya ustawi wa jamii iwafikie wananchi wote ambao wanahitaji, pia amewapongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya..