DKT. HOMERA ATETA NA WANAFUNZI WANAOSOMA QINGDAO, CHINA.
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amekutana na kufanya mazungumzo na wanafunzi wa Kitanzania wanaoendelea na masomo jijini Qingdao, nchini China, ambapo amewahimiza kutumia vyema fursa ya elimu waliyonayo kujipatia maarifa na ujuzi utakaowawezesha kushiriki katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya nishati nchini.
Dkt. Homera amekutana na wanafunzi hayo Novemba 26, 2026, jijini Qingdao, Jimbo la Shandong, nchini China, mara baada ya kushiriki Mkutano wa Nne wa Mawaziri wa Nishati wa Ushirikiano wa Belt and Road (Belt and Road Energy Partnership), unaofanyika kuanzia Novemba 25 hadi 27, 2026.
Wanafunzi hao wanaendelea na masomo katika ngazi mbalimbali za elimu ya juu, kuanzia Shahada ya Kwanza hadi Shahada ya Uzamivu (PhD), katika vyuo mbalimbali jijini Qingdao, ikiwemo Chuo Kikuu cha China Petroleum, kinachojihusisha na mafunzo na tafiti katika sekta ya mafuta na gesi.
Akizungumza na wanafunzi hao, Dkt. Homera amesema Tanzania inaendelea kutekeleza na kujiandaa kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati katika sekta ya nishati, hivyo kuna umuhimu wa kuwa na wataalamu wazalendo wenye ujuzi wa kutosha ili kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje ya nchi na kulinda maslahi ya Taifa.
Ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni Mradi wa Gesi Asilia Kimiminika (LNG) mkoani Lindi, Mradi wa Mini-LNG pamoja na miradi ya uzalishaji wa umeme kwa kutumia makaa ya mawe, upepo, jua na jotoardhi.
“Miradi hii yote inahitaji wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu, na Serikali ina matumaini makubwa kwa vijana wa Kitanzania wanaopata elimu katika maeneo mbalimbali duniani kurejea nyumbani na kutumia maarifa yao katika kuendeleza sekta ya nishati na sekta zingine,” amesema Dkt. Homera.
Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka lengo la kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini hadi kufikia megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030, hatua inayotarajiwa kuongeza mahitaji ya wataalamu wa kada mbalimbali katika sekta ya nishati.
Dkt. Homera ameeleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na mikakati mingine ya maendeleo ya sekta ya nishati utafungua fursa nyingi za ajira kwa wataalamu wa Kitanzania, hivyo amewataka wanafunzi hao kutumia vyema nafasi waliyonayo ya kupata elimu na ujuzi nje ya nchi ili kuchangia maendeleo ya sekta ya nishati na Taifa kwa ujumla.